March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanafunzi wa familia duni Mwanza wapatiwa msaada wa vifaa vya shule

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Mwanza

Taasisi ya The Desk & Chair Foundation katika kupunguza changamoto ya ukosefu wa vifaa vya shule miongoni mwa watoto wanaotoka katika familia imewapatia vifaa vya elimu wanafunzi 1,000 wa shule za msingi na sekondari jijini Mwanza.

Akizuy wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwa baadhi ya wanafunzi hao,Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Alhaji Dkt.Sibtain Meghjee,amesema licha ya serikali kutoa elimu bila malipo, bado baadhi ya wanafunzi wanakabiliwa na changamoto ya kukosa madaftari, sare, viatu na mabegi kutokana na kipato duni cha wazazi na walezi wao.

Amesema kupitia mradi wa kuboresha elimu, wanafunzi 1,000 wanaoendelea na masomo pamoja na wanaoanza masomo watanufaika, ili kuwapa mazingira rafiki ya kujifunzia na kuongeza ari ya masomo.

Dkt.Meghjee ameishauri serikali kupunguza au kuondoa kodi kwenye vifaa vya elimu ili taasisi hiyo iweze kuwahudumia wanafunzi wengi zaidi, akibainisha kwa zaidi ya miaka 10, imekuwa ikitoa huduma kwa jamii bila kubagua kupitia kauli mbiu ya “Tupo Pamoja, Iwe Dhiki Iwe Faraja”.

Baadhi ya wazazi wa wanafunzi walionufaika waliishukuru taasisi hiyo na kuiomba serikali kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya kusaidia watoto wenye ulemavu wanaotoka katika familia zenye changamoto ya ulemavu ikiwemo kupata vifaa vya shule na haki ya elimu.

Mkazi wa Igombe wilayani Ilemela mkoani Mwanza, Emmanuel Daud,amesema hali yake ya ulemavu na kipato kidogo kinachotokana na kilimo cha kujikimu vinamfanya ashindwe kumudu gharama za vifaa vya shule kwa watoto wake, hivyo akaomba serikali iangalie kundi hilo kwa jicho la huruma.

Pia, mkazi wa Pasiansi wilayani Ilemela, Baraka Obwele mwenye ulemavu wa miguu, amesema serikali iwaangalie walemavu pamoja na watoto wao wapate haki ya elimu watimize ndoto zao.

“Nimshukuru Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation kwa moyo wake wa kusaidia jamii, ameendelea kuwawezesha watoto vifaa vya elimu, nina watoto watatu na hapa amenisaidia mmoja. Serikali sisemi imeshindwa la, ituangalie walemevu watoto wetu wapate elimu sawa na wengine,”amesema.

Kwa upande wao wanafunzi walionufaika akiwemo Mariam Said wa Mlimani Sekondari, Latifa Ramadhan wa Ibungilo Sekondari na Mwanaisha Hassan wa Shule ya Msingi Sahara, walisema msaada huo umeongeza morali na motisha ya kusoma kwa bidii.

“Hali duni ya kiuchumi imekuwa kikwazo kwa baadhi ya wazazi kumudu gharama za kununua vifaa vya shule kwa ajili ya watoto wao, licha ya kuwa wana mwamuko wa elimu.Serikali irejeshe utaratibu wa zamani madaftari yapatikane shuleni, wazazi wabaki na jukumu la kununua sare na viatu,”ameshauri Mariam.

Jumla ya shilingi milioni 15 zilitumika kununua katoni 354 sawa na madaftari zaidi ya 5,500 pamoja na mabegi 300, ambapo awamu ya kwanza wanafunzi 1,000 wamenufaika na awamu ya pili ya msaada huo inatarajiwa kutolewa mwishoni mwa wiki ijayo.