Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Tabora
WATU wawili wamepoteza maisha kwa kupigwa na radi wakiwa wamejikinga mvua kwenye kibaraza cha nyumba yao iliyoegemewa na mti kijiji cha Songambele, Kata ya Uyowa,wilayani Kaliua mkoani Tabora.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora SACP.Richard Abwao amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Desemba 27 mwaka huu ambapo amesema mbali na waliopoteza maisha watu wengine wawili walijeruhiwa.
Ametaja waliopoteza maisha kuwa ni Mwagala Marando (19) na Moses Lwega (20) wakulima, wakazi wa kijiji hicho na waliojeruhiwa ni Yohana Peter (18) na George Deusi (18), na wanaendelea kupatiwa matibabu kwenye kituo cha afya.
Abwao ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari hasa katika kipindi hiki ambacho mvua zimeendelea kuongezeka na kuwataka wajikinge katika maeneo yaliyo salama ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.
Katika tukio jingine Kamanda huyo,amesema mwili wa mwanaume mmoja aliyefahamika kwa jina la Hamis Ramadhan, mkazi wa Kata ya Isevya, dereva wa bodaboda, umeokotwa katika mtaro wa maji machafu uliopo Mtaa wa Malolo Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.
Abwao ameeleza kuwa uchunguzi wa kisayansi unaendelea kufanyika ili kubaini chanzo cha kifo hicho na watatoa taarifa kwa umma, mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Tabora ya Kitete.
Mbali na uchunguzi huo amesema kuwa jitihada za kupata pikipiki ya marehemu huyo zinaendelea,hivyo amewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kufanikisha uchunguzi na kupatikana pikipiki hiyo.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi