Na Agnes Alcardo, TimesMajira Online, Dar es Salaam
LICHA ya mvuto wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na serikali kupitia Halmashauri,wananchi wameshauri iangaliwe namna ya kupunguza kiwango cha marejesho ili kuwezesha wanufaika kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.
Mikopo hiyo ya asilimia 10 inatolewa kwa vikundi vilivyosajiliwa vya wanawake asilimia 4, vijana asilimia 4 na watu wenye ulemavu asilimia 2,
Ikumbukwe kuwa hivi karibuni serikali ilirejesha utoaji wa mikopo ya asilimia 10baada ya kufanya maboresho mbalimbali, huku ikisisitiza kuwa sasa itatolewa kupitia mfumo wa benki.
Mbali na ushauri huo, wanufaika wameomba pia kuwezeshwa elimu kuhusu taratibu za uombaji wa mikopo pamoja na matumizi sahihi ya fedha hizo ili waweze kurejesha madeni bila changamoto.
Kupitia ombi hilo, taasisi ya Women of Influence (WOI) kupitia mradi wake wa Kilinge cha Sheria, wenye lengo la kuwasaidia wanawake kujikwamua kiuchumi, iliamua kuibeba agenda hiyo kwa kusaidia vikundi vinavyokusudia kuomba mikopo ya serikali.
Kikundi cha Mkombozi, chenye jumla ya wanakikundi saba, ni miongoni mwa vikundi vilivyonufaika na mradi huo kwa kusaidiwa kupata mkopo, hatua ambayo wanakikundi hao wanaisifu kuwa imeleta manufaa.
Miongoni mwa msaada walioupata kupitia Kilinge cha Sheria ni kuandaliwa maandiko muhimu, katiba ya kikundi, urasimishaji wa kikundi pamoja na maandalizi ya nyaraka zote zinazohitajika ili kustahili kupata mkopo.
Hatua ya WOI kujitolea kusaidia wanavikundi hao imetokana na uelewa wao kwamba wapo Watanzania wengi wenye uhitaji wa mikopo hiyo, lakini wanashindwa kuiomba kutokana na ukosefu wa elimu juu ya taratibu za uombaji.
Silvia Alphonce, mwanakikundi wa Mkombozi na mnufaika wa Kilinge cha Sheria, anasema lengo la kikundi chao kuomba mkopo wa serikali ni kujikwamua kiuchumi.
“Ninaishukuru serikali kwa kurejesha mikopo ya asilimia 10, lakini pia ninaishukuru Kilinge cha Sheria kwa kutuwezesha na kutusaidia kupata mikopo hiyo.Wametusaidia kupata namba ya mlipa kodi (TIN) pamoja na nyaraka zote zilizohitajika,” anasema Silvia.
Hata hivyo, Silvia anabainisha kuwa walikumbana na changamoto katika mchakato wa uombaji, ikiwemo kutowekwa wazi kwa vigezo vyote vinavyohitajika, hali iliyosababisha kutumia muda mrefu kabla ya kupata mkopo.
“Wito wangu kwa serikali ni kuweka wazi mchakato wa utoaji wa mikopo ili mwananchi ajue mapema mahitaji yote, na kuendelea kutoa elimu kuhusu mikopo ya asilimia 10,” anashauri.
Aidha, anawahimiza wanawake wajasiriamali kujitokeza kuomba mikopo hiyo kwa kufika serikali za mitaa na kuifuatilia, akisema itawasaidia kuinuka kiuchumi na kufikia malengo yao.
“Ninashukuru Kilinge cha Sheria kwa uvumilivu na elimu waliotupatia. Waendelee kutusaidia kwa kuwa serikali pekee haiwezi, kuna watu wengi wanahitaji msaada wa karibu,” anasema.
Mnufaika mwingine, Zuhura Juma, anaishukuru serikali kwa kutoa mikopo hiyo pamoja na Kilinge cha Sheria kwa kuwawezesha kuipata.
“Hali ya maisha kwa sasa ni ngumu. Mikopo hii imekuja wakati mwafaka, lakini naomba serikali iangalie namna ya kupunguza kiwango cha marejesho,kwa mfano, mimi natakiwa kurejesha shilingi laki mbili kwa mwezi kwangu ni kiasi kikubwa ukizingatia ugumu wa biashara,” anasema.
Anasema wapo wanufaika wengi wanaorejesha kiasi kikubwa zaidi huku mazingira ya biashara yakiwa magumu, hivyo anaomba eneo hilo liangaliwe kwa kina.
Mnufaika mwingine, Frola Chiwalanga, anasema mikopo hiyo ni mizuri kwa kuwa inaambatana na elimu ya namna ya kutumia fedha na kurejesha deni kabla ya kutolewa.
“Changamoto ni ufuatiliaji unaochukua muda mrefu, lakini tunawahimiza wanawake wajitokeze kuomba mikopo hiyo kwani inaweza kuinua maisha yao na kuwasaidia kupiga hatua,” anasema.
Mkurugenzi Mtendaji wa WOI,Doreen kalugira,anasema mbali na kusaidia upatikanaji wa mikopo, taasisi hiyo pia inajihusisha na kutokomeza ukatili wa kijinsia nyumbani na rushwa ya ngono kupitia uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake.
Anasema WOI huwasaidia wanawake wajasiriamali kukuza biashara zao kwa kuwaunganisha na mitaji, mikopo rafiki pamoja na fursa mbalimbali za kiuchumi.
Kwa mujibu wa Doreen, taasisi hiyo imeleta mageuzi kwa wanawake wajasiriamali wadogo kwa kuwapa taarifa sahihi kuhusu mikopo isiyo na riba, kuwasaidia kutimiza vigezo, kuwajengea uwezo wa kibiashara na kuwaongoza katika taratibu za kisheria za usajili wa biashara.
Anasema hadi sasa WOI imefanikiwa kusaidia vikundi viwili vya Mkombozi na Nange vilivyopo Kigogo, Dar-es-Salaam kupata mikopo ya asilimia 10 yenye jumla ya milioni 39.5 kutoka mfuko wa mikopo ya serikali isiyo na riba.
“Baada ya mikopo kuidhinishwa, tunaendelea kuviongoza vikundi hivyo hadi kupata vyeti vya ulipaji kodi na leseni za biashara, hatua muhimu katika kuhalalisha biashara zao,” anasema.
Anabainisha kuwa juhudi hizo zimewezeshwa kwa msaada wa Women First International, taasisi ya Kimarekani inayounga mkono uwezeshaji wa wanawake nchini Tanzania.
Aidha, WOI imebuni programu ya simu iitwayo Kilinge Digital, inayotoa taarifa za mikopo rafiki kutoka taasisi mbalimbali za kifedha nchini, lengo likiwa kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi hasa kwa wanawake wajasiriamali.
“Tunataka kuona wanawake wakipata mitaji ya kuanzisha na kukuza biashara zao. Tukiwapa taarifa, ujuzi na mitaji rafiki, tunainua familia zao na uchumi wa taifa,” anasema Doreen.
Anahitimisha kwa kusema uwezeshaji wa wanawake si suala la mikopo pekee, bali ni safari ya kujenga misingi imara ya kiuchumi itakayosaidia kupunguza ukatili wa kijinsia katika jamii.
“Wanawake wanapokuwa na uwezo wa kifedha, wanaweza kuhudumia familia zao na kuwasomesha watoto wao,” anasema huku akiwaomba wadau wengine kuunga mkono juhudi hizo.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina