March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa VEMA kuchochea ajira kwa vijana Mwanza

*Ni baada ya vijana 171 kuhitimu mafunzo ya ufundi stadi mbalimbali


*Kupitia mafunzo hayo 28 waajiriwa,20 wajiajiri

Na Judith Ferdinand
TimesMajira Online – Mwanza

Vijana 171 kutoka Wilaya za Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza wamefanikiwa kupata ujuzi mbalimbali wa ufundi stadi kupitia mafunzo yatawawezesha kujiajiri na kuchochea uchumi pamoja na maendeleo ya taifa.

Vijana hao wamenufaika na mafunzo hayo kupitia Mradi wa Vijana Elimu, Malezi na Ajira (VEMA) unaotekelezwa katika wilaya za Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza na Shirika la Plan International, kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ubelgiji (DGD).

Akizungumza Desemba 17, 2025 katika mahafali ya kwanza ya mafunzo ya ufundi stadi yaliyofanyika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Mkoa wa Mwanza, Mratibu wa Mradi wa VEMA kutoka Plan International, Gadiely Kayanda, amesema mradi huo una malengo makuu matatu ambayo ni elimu jumuishi, uwezeshaji wa vijana kiuchumi, pamoja na ulinzi wa mtoto na kupinga ukatili wa kijinsia.

Kayanda amesema katika lengo la kuwawezesha vijana kiuchumi, shirika hilo linashirikiana na Shirika la SEDIT pamoja na VETA Mwanza, kwa lengo la kuwapatia vijana ujuzi unaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.

Ameeleza kuwa jumla ya vijana 800 wamenufaika na mradi huo kwa awamu tatu, ambapo hadi sasa awamu mbili tayari zimehitimu mafunzo ya nadharia na vitendo katika fani mbalimbali ikiwemo ushonaji, ufundi mabomba, upishi na nyinginezo.

Amefafanua kuwa mafunzo hayo yalitolewa kwa namna mbili, ambapo kijana alikuwa na uhuru wa kuchagua kusoma kwa fundi mahiri aliye karibu na makazi yake au kuhudhuria mafunzo VETA Mwanza kila siku.

“Katika awamu hii ya kwanza vijana 200 walisajiliwa kwa ajili ya mafunzo ya ufundi stadi, kati yao 171 wamefanikiwa kuhitimu sawa na asilimia 85.5. Hii ni hatua kubwa katika kuwawezesha vijana kiuchumi. Tulitumia shilingi milioni 80 kulipia ada za mafunzo pamoja na kununua vifaa vya kujifunzia. Aidha, vijana waliomaliza mafunzo katika vikundi vya uzalishaji tumewapatia vifaa vya kuanzia kazi kulingana na fani walizosoma vyenye thamani ya shilingi milioni 40,” amesema Kayanda.

Ameongeza kuwa kutokana na ujuzi walioupata, vijana takribani 28 wameajiriwa katika kampuni binafsi zikiwemo hoteli, gereji na karakana za uchomeleaji huku wengine 20 wamefanikiwa kujiajiri.

Sanjari na hayo, Kayanda amesema mradi umefanikiwa kuunda vikundi 53 vya kuweka akiba na kukopa vyenye jumla ya vijana 1,158, wakiwemo wanawake 633, wanaume 525 pamoja na watu wenye mahitaji maalumu.

Ameeleza kuwa vijana hao wamepatiwa pia mafunzo ya elimu ya fedha, ujasiriamali, biashara, kuweka akiba na kukopa, usawa wa kijinsia pamoja na matumizi ya teknolojia ya kidijitali.

“Hadi sasa vikundi hivyo vimefanikiwa kuweka akiba ya zaidi ya shilingi milioni 192.9, ambapo kati ya hizo zaidi ya shilingi milioni 107.3 zimetumika kutoa mikopo kwa wanachama wao kwa ajili ya kuanzisha biashara. Jumla ya biashara 809 zimeanzishwa, zikiwemo 441 zinazoendeshwa na wanawake na 368 na wanaume,” amesema.

Hata hivyo, Kayanda ametaja changamoto zilizojitokeza kuwa ni pamoja na utoro wa baadhi ya wanafunzi uliosababishwa na majukumu ya kifamilia, hali iliyosababisha baadhi yao kuacha mafunzo. Ameeleza kuwa katika awamu ya kwanza, wanafunzi watano wa kike walijifungua wakati mafunzo yakiendelea.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha VETA Mwanza, Mhandisi Henry Kasele, amesema mradi wa VEMA ulianza Machi 2024 ukiwa na lengo la kuwasaidia vijana 800 kutoka kata 13 za Wilaya za Ilemela na Nyamagana kupata ujuzi wa ufundi stadi katika fani mbalimbali ikiwemo umeme wa magari, ufundi magari, uchomeleaji, umeme wa majumbani, ushonaji, usalama pamoja na upishi.

“Wanufaika wa mradi huu ni vijana wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi, hivyo mradi huu ni suluhisho la kuwapatia fursa za kujiajiri na kuajiriwa ili waweze kujikwamua kiuchumi,” amesema Mhandisi Kasele.

Naye Jesca Kanuti, mnufaika wa mradi wa VEMA, amesema kupitia mafunzo hayo wamefanikiwa kujiajiri kwa kufungua ofisi ya ufungaji mabomba, wakitoa huduma ya kufunga mifumo ya maji safi na maji taka kwenye nyumba.

“Mradi huu umenisaidia kuanza kujiwekea akiba na kuondokana na utegemezi. Awali sikuweza hata kujiwekea akiba ya shilingi 500, lakini sasa naweza kujihudumia mahitaji yangu ya msingi na kusaidia familia yangu,” amesema Jesca.

Jesca ameomba Serikali na wadau wa maendeleo kuwawezesha vijana kwa mikopo ili waendelee kujikwamua kiuchumi kupitia ujuzi walioupata.

Kwa upande wake Ofisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa Asasi za Kiraia wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Yusuph Omollo, amesema halmashauri inatoa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia vikundi au mtu mmoja mmoja ndani ya kikundi.

“Ameeleza kuwa marejesho ya mikopo ni lazima kwani si ufadhili bali ni mkopo. Amesisitiza kuwa baadhi ya wananchi hukosa mikopo kwa kushindwa kukidhi vigezo, hivyo Maofisa Maendeleo wa Kata wanapaswa kusaidia vikundi kusajiliwa na kujiunga na mfumo rasmi,” amesema Omollo.

Baadhi ya wahitimu wa mafunzo ya stadi yaliotolewa na VETA kupitia mradi wa VEMA unaotekelezwa na shirika la Plan International