March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kituo cha afya Kiyombo chapatiwa gari la wagonjwa

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online -Sikonge

SERIKALI imepeleka gari jipya la kuhudumia akinamama wajawazito na wagonjwa wengine katika Kituo cha Afya cha Kiyombo kilichoko katika Kata ya Kipili wilayani Sikonge, mkoani Tabora.

Akikabidhi gari hilo Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Thomas Myinga,amesema gari hilo jipya lenye vifaa tiba ndani ni mkombozi kwa wananchi hao ambao walikuwa wanapata tabu kufuata huduma ya afya kwa umbali wa zaidi ya km 300 mpaka makao makuu ya Wilaya.

“Wajawazito na wagonjwa waliokuwa wanahitaji huduma za haraka na rufaa kwenda hospitali kubwa,walikuwa wanahangaika namna ya kwenda kwa kukosa usafiri hali iliosababisha baadhi yao kupoteza maisha,”amesema Myinga.

Mbunge wa Jimbo la Sikonge Mhandisi Amos Maganga,amesema kuwa gari hilo ni sehemu ya mikakati ya serikali ya kuhakikisha huduma za kijamii zinaboreshwa katika sekta zote ili kumaliza kero za wananchi.

Hivyo Mhandisi Maganga,ametoa wito kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo,Seleman Pandawe na Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Christopher Nyalu kuhakikisha gari hilo linatumika kwa kazi iliyokusudiwa ya kubeba wagonjwa wa dharura ili wawahishwe hospitalini.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ya Sikonge,Andrea Lwambano na Diwani wa Kata ya Kipili Daniel Gudi wamemhakikishia Mkuu wa Wilaya na Mbunge wa Jimbo hilo kuwa gari hilo ili litatumika kutoa huduma kwa wagonjwa na wajawazito wa kata hiyo na maeneo mengine.