Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online- Mbozi.
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe, wamekumbushwa kusimamia majukumu yao bila kujihusisha na vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha mgongano wa maslahi ambao umekuwa chanzo cha kudhoofisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Rai hiyo ilitolewa Desemba 5, 2025 na Ofisa Uchunguzi Mkuu kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Majid Mohamed, mara baada ya Madiwani kula kiapo katika mkutano wa kwanza uliofanyika shule ya sekondari ya kutwa Vwawa wilayani humo.

Mohamed alisema Madiwani hawapaswi kushiriki au kujihusisha kwa namna yoyote na zabuni zinazotangazwa na Halmashauri, kwani kufanya hivyo kunahatarisha uwazi na haki .
Aidha, amewakumbusha kuwa zawadi wanazopokea baada ya kuwahudumia wananchi hazipaswi kuzidi kiasi cha shilingi 200,000, na endapo zitazidi kiwango hicho wanapaswa kuwasilisha taarifa kwa Mkurugenzi ili ziwekwe kwenye mpango rasmi wa matumizi.
Baada ya kuhitimishwa kwa zoezi la kiapo, Madiwani wa Halmashauri hiyo, wamemchagua Diwani wa Kata ya Halungu, Maarifa Mwashitete, kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri, akiibuka na kura zote 40.
Baraza hilo lilitarajiwa kuwa na madiwani 41, lakini idadi hiyo ilipungua kufuatia kifo cha Diwani mteule wa Kata ya Shiwinga aliyefariki dunia siku chache kabla ya kuapishwa, kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kunywa maji ya betri.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbozi, Mbwana Kambangwa, alimtangaza pia Diwani wa Viti Maalum, Fausta Kibona kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, naye akijizolea kura zote 40.
Akizungumza mara baada ya kufungua kikao cha kwanza cha baraza hilo, Mwashitete,ameahidi kusimamia kwa kasi ukusanyaji wa mapato inayoendana na matumizi sahihi ya fedha hizo zilizokusanywa.
Aidha amesema,hatavumilia uzembe katika utekelezaji wa majukumu ya ukusanyaji mapato.

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega, amewataka Madiwani kufanya kazi kwa ushirikiano na watumishi kama timu moja ili kuisukuma mbele Halmashauri hiyo.
Mbega amesisitiza umuhimu wa Madiwani kutanguliza maslahi ya wananchi na kutunza siri za vikao, sanjari na kujiepusha na vitendo vinavyowavunjia heshima kama matumizi ya lugha chafu na ulevi.


More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako