March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Senyamule atangaza siku tatu za maombi ya amani Dodoma

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online, Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ameongoza viongozi wa dini katika maombi maalumu ya kuombea amani ya mkoa huo na Taifa kwa ujumla , huku akitangaza siku tatu za maombi kwa wananchi wote wa Dodoma ili kumlilia Mungu kwa ajili ya utulivu na ustawi wa mkoa huo na nchi.

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuhimarisha mshikamano na kuleta utulivu baada ya matukio ya vurugu yaliyoshuhudiwa wakati wa uchaguzi.

Akizungumza katika kikao maalumu kilichowakutanisha viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali, Senyamule amesema maombi hayo yataanza Disemba 7-9 mwaka huu kwa Kila mmoja mahali alipo kumlilia Mungu Kila mmoja kwa dini yake.

“Naomba mkawatangazie na waumini wenu kuwa tutakuwa na maombi ya siku tatu kuanzia Disemba 7-9 mwaka huu ,Kila mmoja kwa dini yake iwe ni kwa kufunga na kuomba Ili mradi tumlilie Mungu kwa pamoja kwa ajili ya mkoa wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla “amesema Senyamule

Amebainisha kuwa maombi hayo ni muhimu katika kipindi hiki ambacho wananchi wanahitaji faraja, umoja na mwelekeo mpya wa kujenga Taifa lenye mshikamano.

Aidha, Mkuu huyo wa mkoa ameeleza kuwa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba 29, siku ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, pamoja na siku chache baada ya uchaguzi, yalileta taharuki kwa wakazi wa maeneo kadhaa ikiwemo mkoa wa Dodoma.

Amesema ni wajibu wa viongozi na wananchi kushikamana ili kuondoa athari za kiakili na kijamii zilizojitokeza kutokana na matukio hayo.

Senyamule amewaasa viongozi wa dini kuendelea kutoa elimu ya amani, ustahimilivu na umuhimu wa kutatua migogoro kwa njia za mazungumzo.

Amesema serikali ya mkoa itaendelea kushirikiana na taasisi za kidini katika kuhakikisha kuwa misingi ya amani na utulivu inaimarika zaidi.

Aidha, Senyamule amesisitiza kuwa amani ni jukumu la kila mwananchi, na kuitaka jamii nzima ya Dodoma kushiriki ibada na maombi hayo maalumu kwa moyo mmoja.

Amesema kuwa mkoa wa Dodoma una nafasi kubwa ya kuendelea kuwa mfano wa utulivu nchini endapo wananchi wataendelea kushikamana na kudumisha maadili ya amani.