Na Esther Macha,TimesMajiraOnline,Mbeya
KATIBU TawalaWilaya ya Mbeya, Mohamed Azizi, ameagiza madiwani pamoja na viongozi wa vijiji na kata kufanya mikutano na vijana, wazee na makundi mengine ili kuwaelimisha kuhusu maana na umuhimu wa amani, akisema amani ndiyo msingi wa maendeleo katika Taifa lolote.
Azizi ametoa maagizo hayo Desemba 3, 2025 wakati wa mafunzo kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma kwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, yaliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu namna taratibu za manunuzi zinavyotekelezwa katika halmashauri zao.
“Niwasisitize ndugu zangu madiwani, mkaitangaze amani. Nendeni mkafanye mikutano na wazee, vijana na makundi mengine ili kuzungumzia amani, ambayo ndiyo matokeo ya kila kitu ndani ya Taifa letu na mataifa mengine,” amesema.

Ameongeza kuwa viongozi wanapaswa kutenga muda wa kutoa elimu juu ya thamani ya amani, akisisitiza kuwa bila amani hakuna huduma, maendeleo wala ustawi wa jamii.
Aidha, Azizi amewataka madiwani kutekeleza majukumu yao kwa weledi, kuwajibika ipasavyo na kuzingatia taratibu za kiutumishi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Kwa upande wake, Meneja wa Manunuzi wa Nyanda za Juu Kusini,Paschal Manono ameleza jinsi walivyotoa elimu kwa madiwani kuhusu taratibu sahihi za manunuzi, uwazi katika matumizi ya fedha za umma, na umuhimu wa kufuata sheria za manunuzi ili kuepuka changamoto zinazoweza kuathiri utendaji.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ambaye pia ni Diwani wa Utengule Usongwe, Aida Haule, amesema mafunzo hayo yataboresha kwa kiasi kikubwa utendaji ndani ya halmashauri, huku akiahidi kuwa madiwani watayatumia kikamilifu katika kusimamia miradi ya maendeleo.
Haule amesema mafunzo hayo, yaliyogusia masuala ya rushwa, maadili na manunuzi, yatatoa dira na mwongozo kwa madiwani katika kutekeleza majukumu yao kwenye kata mbalimbali.
“Niwaase waheshimiwa madiwani, tutekeleze mafunzo haya. Tuna vijana wengi katika maeneo yetu, hivyo tushirikiane nao kwa karibu ili kuleta matokeo chanya,” alisema.


More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi