Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Bukoba
TAKWIMU za udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano mkoani Kagera zimeendelea kupungua kutoka asilimia 41 hadi 39 kwa mwaka 2019 kutokana na wananchi kuendelea kuwa na mtazamo chanya kuhusu malezi ya watoto chini ya miaka mitano ikiwemo unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee mtoto anapijifungua mpaka kufikia umri wa miezi 6.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa uhamasishaji na uelimishaji maswala ya afya mkoa wa Kagera, Ndugu Nelison Rumbeli wakati wa shughuli ya wakina mama wenye watoto chini ya miezi sita iliyopewe jina la “Mother Meet up” ikimaanisha kina mama kukutana iiyofanyika jana katika ukumbi wa Bijampora kata ya Kemondo halmashauri ya Bukoba.
Shughuli hiyo iliyoandaliwa na serikali kwa ushirikiano na mradi wa USAID Tulonge afya kupitia jukwaa la NAWEZA ilihusisha ushiriki wa akina mama wenye watoto chini ya miezi 6 zaidi ya 50.
Amesema kwa miaka mitano iliyopita kiwango cha udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano kilikuwa asilimia 41 ila kwa mwaka 2019 kiwango hicho kimeshuka na kufikia asilimia 39.
Kushuka kwa kiwango hiki ni kutokana juhudi na msukumo wa serikali ya awamu ya tano katika kuboresha Sekta ya Afya.Pia Serikali imeendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ikiwemo USAID Tulonge Afya katika kuhamasisha maelezi bora kwa watoto kuanzia kipindi cha kuzaliwa mpaka anapofikisha umri wa miaka mitano.
Rumbeli amesema waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo alizindua na kusainiana mikataba na wakuu wa mikoa, na ngazi mbali mbali za uongozi hadi ngazi ya vijiji lengo likiwa ni kushughulikia swala la lishe kwani ni jambo kubwa lililokuwa linasumbua maeneo mbalimbali hapa nchini.
Ameongeza kuwa, vifo vya mama vinavyojitokeza wakati wa kujifungua mwaka jana vilikuwa 80 kwa mkoa wa Kagera na mwaka huu vifo hivyo vimepungua ambapo hadi sasa ni vifo 45. Kupungua kwa vifo hivyo kumetokana na ongezeko la ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na dispensary pamoja na ongezeko la madawa katika hospitali hizo. Lakini pia uhamiasishaji na elima waliyopatiwa wakina mama juu ya umuhimu wa kuhudhuria kliniki pindi wanahisi ujauzito.
Kwa upande wa mratibu wa mradi wa USAID Tulonge Afya ngazi ya wilaya kutoka shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na maswala ya afya na mazingira (TADEPA) Benson Rweyemamu alisema kuwa, lengo la “Shughuli ya Mother Meetup” ni kutoa nafasi kwa akina mama wenye watoto chini ya miezi 6 kujadiliana na kupeana uzoefu juu ya malezi ya mtoto kuanzia kipindi anazaliwa mpaka kufikisha umri wa miaka 5 na kuwafanya wao pia kuwa Mabalozi wazuri kwenye jamii zao.
Mambo muhimu yaliyojadiliwa kwenye shughuli hii ni unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi 6 kutokea mtoto anapozaliwa, kufuatilia matibabu kwa wataalam wa Afya pindi wanapohisi mtoto anatatizo, kulala kwenye chandarua chenye dawa na matumizi ya njia za kisasa za afya ya uzazi.
Rweyemamu ameongeza shughuli hiyo ya “Mother Meetup” hufanyika kila baada ya miezi sita na walengwa ni wakina mama wenye watoto chini ya miezi sita. Katika shughuli ya leo waalikwa wametoka katika kata saba za halamshauri ya Bukoba ambazo ni za Maruku, Kemondo, Kanyangereko, Katerero, Karabagaine, Nyakato na Katoro.
Naye Meneja mradi wa Tulonge afya kwa kanda ya ziwa Sihiana Mkanda amesema Tulonge Afya ni mradi wa miaka mitano unaotekelezwa kwa ufadhili wa shirika la kimarekani la USAID kwenye mikoa 12 nchini Tanzania. Kwa upande wa kanda ya Ziwa mradi unatekelezwa katika mikoa ya Mwanza,Geita,Kagera,Mara,Shinyanga na Kigoma.
Amesema katika mikoa ya kanda ya ziwa mradi huo uko katika wilaya 12 na kwa mkoa wa Kagera ni katika wilaya za Muleba na Bukoba vijijini na kuwa walichagua wilaya hizo kutokana na changamoto ya afya walizokuwa nazo wanajamii wa wilaya hizo.
Mmoja wa wakina mama walioshiriki kwenye shughuli ya Mother Meetup Shemsa Nasoro amesema Katika shughuli hiyo amejifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na faida za kunyonyesha mtoto miezi sita tangu anapozaliwa bila kumpa kitu chochote, kumpeleka kituo Cha afya mara tu anapougua na matumizi ya njia njia za kisasa za Afya ya uzazi.
“Na mimi nikitoka hapa ntaenda kuwaeleza wakina Mama wenzangu ambao hawakuweza kufika hapa yote niliyojifunza leo ili tuweze kuwa na jamii yenye afya bora” amesema Shemsa
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea