March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TGS kuendeleza migodi ya wachimbaji wadogo

Na Esther Macha,TimesMajiraOnline,Mbeya

RAIS wa Chama cha Wanajiosayansi Tanzania (TGS), Prof. Elisante Mshiu amesema wataalamu wa jiolojia nchini wanaendelea kutoa mchango mkubwa katika kuendeleza migodi ya wachimbaji wadogo pamoja na kusaidia upatikanaji wa rasilimali za mafuta na gesi.

Akizungumza Desemba 3, 2025 wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa TGS uliofanyika jijini Mbeya, Prof. Mshiu amesema  mkutano huo umehusisha zaidi ya wanajiosayansi 4,000 kutoka wizara mbalimbali, taasisi za Serikali na vyuo vikuu.

“Mkutano huu umekutanisha taasisi nyingi kutoka maeneo mbalimbali nchini, lengo likiwa kujadili kwa kina sekta hii muhimu,”amesema .

Aidha, Prof. Mshiu alibainisha kuwa TGS inaendelea kushirikiana na jumuiya za kimataifa na kikanda kama zile za Afrika Mashariki—ikiwemo Kenya na Uganda—ili kunufaika na fursa mbalimbali za kitaalamu na kiteknolojia.

Hata hivyo, amesema licha ya mchango mkubwa wa wataalamu katika ugunduzi wa rasilimali, bado kuna changamoto ya kuzifanyia kazi ipasavyo, pamoja na kuchelewa kukamilika kwa mchakato wa usajili wa bodi ya wataalamu hao.

“Tumepiga hatua kupitia kamati maalum, lakini bado tunahitaji mchakato wa bodi hiyo kukamilika ili tuendelee kuchangia kikamilifu katika kufikia Dira ya Maendeleo Endelevu 2050,” ameeleza .

Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mbeya anayeshughulikia Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bi. Anna Mwambene, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Beno Malisa, amewataka
wanajiosayansi kuongeza utafiti wa kina wa udongo na miamba ili kuzuia madhara yanayowapata wachimbaji wadogo.

Amesema hali ya kijiolojia ukifanyika kwa ufanisi utawasaidia wachimbaji wadogo kuongeza uzalishaji na kutoacha shughuli zao kutokana na kukata tamaa.

“Utafiti wa kina utawasaidia wachimbaji kuipenda kazi yao bila kukata tamaa na pia kupanua maeneo mapya ya uchimbaji,” amesema.

Mwambene ameongeza kuwa Mkoa wa Mbeya unashika nafasi ya pili kitaifa kwa uzalishaji wa dhahabu, hivyo matokeo ya mkutano huo yanapaswa kusaidia mkoa huo kupanda hadi nafasi ya kwanza.