Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Benki ya Access nchini imezindua rasmi Access Wezesha, jukwaa jipya linalolenga kuwawezesha vijana wa kizazi kijacho kupata maarifa muhimu ya uelewa wa masuala ya fedha. Benki imeshirikiana na AIESEC IFM kuendesha mafunzo ya kina ya elimu ya fedha kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, ambapo zaidi ya vijana 200 walihudhuria ili kujifunza kuhusu akiba, upangaji bajeti, na kukuza tabia bora za usimamizi wa fedha.
Hatua inaonyesha dhamira ya Access Bank katika kuongeza ujumuishwaji wa kifedha na kuwawezesha vijana kupitia elimu na huduma rafiki za kibenki. Kupitia ajenda hii, Benki pia imeunda Akaunti ya IZE, akaunti mahsusi kwa vijana itakayo wasaidia wanafunzi kusimamia fedha zao kwa urahisi na uwajibikaji.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Irene Mutiganzi, Mkuu wa Masoko na Mawasiliano ya wa Kampuni katika Access Bank Tanzania, alisisitiza umuhimu wa kuwafundisha vijana masuala ya fedha mapema.
“Kuwawezesha vijana kupitia elimu ya fedha ni hatua muhimu katika kuhakikisha mustakabali wao. Wanapofahamu namna ya kuweka akiba, kupanga bajeti, na kusimamia fedha zao kwa uwajibikaji, wanakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kufikia malengo yao.

Ushirikiano wetu na AIESEC IFM unaonyesha dhamira yetu ya kuunga mkono ukuaji na maendeleo ya vijana nchini,”amesema
Akizungumza katika tukio hilo, Faith Jonas Kwayu, Rais wa Tawi la AIESEC IFM, amesema ushirikiano huu na Access Bank unaendana kikamilifu na dhamira yao ya kuwaandaa vijana kukabiliana na changamoto za dunia halisi.
“Uelewa wa fedha ni msingi muhimu wa uongozi wenye uwajibikaji na ukuaji binafsi. Tunajivunia kuona vijana wengi wakichukua hatua hii kuelekea kujenga maisha salama na yenye uwezeshaji.”amesema
Mafunzo hayo yalijumuisha vipindi shirikishi, mazoezi ya kupanga bajeti, na majadiliano yaliyolenga kuwasaidia washiriki kufanya maamuzi sahihi ya kifedha.
Access Bank na AIESEC wamethibitisha tena dhamira yao ya kuendeleza programu kama hizi katika maeneo mbalimbali nchini katika juhudi za kuunga mkono maendeleo ya vijana.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako