March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TARA yaomba kutambulika kibingwa na kibobezi

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

CHAMA Cha Wataalam wa Radiografia Tanzania(TARA)kimeiomba Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuangalia namna ya kutatua changamoto ya kitaaluma ya kutotambulika kwa huduma za kibingwa na kibobezi kama ilivyo kwenye kada nyingine za afya.

Ombi hilo limetolewa jijini hapa leo Novemba 27 ,2025 na Rais wa Chama hicho Bakary Msongamwanja,wakati akisoma risala ya chama hicho kwenye ufunguzi wa Kongamano la kisayansi na Mkutano Mkuu unaokwenda sambamba na kaulimbiu isemayo  “Wezesha Mhudumu wa Afya Kupitia Vipimo Bora”(Empowering healthcare through imaging Excellence)”.Ambapo amesema pamoja na mafanikio waliyo nayo kada hiyo imekuwa na changamoto yakutotambulika kwa huduma za kibingwa na bobezi tofauti na kada zingine zinavyotambulika.

Hivyo Msongamwanja ameiomba serikali kuanzisha programu zikatazotoa Elimu ya Shahada ya Uzamili katika masuala ya Radiografa kupitia vyuo vya ndani,

Ambapo amesema hatua hiyo itawawezesha kuongeza Elimu na kujipatia ujuzi wa masuala ya Radiografa na hatimaye kuwekwa kwenye nafasi za kibingwa na ubobezi kama zilivyo kada zingine za Afya.

“Kama unavyofahamu ongezeko la elimu ni kubwa na teknolojia inakuwa kwa kasi siku kwa siku matumizi ya Akili Unde yamekuwa ndio teknolojia ya kisasa hivyo hatuna budi kuongezewa wigo wa kujiendeleza kielimu kupitia vyuo vyetu vya ndani kwani gharama ya kusoma nje ya Nchi ni kubwa na ni wachache wanaweza kumudu gharama hizo,”amesema Msongamwanja.

Pamoja na hayo amesema wao kama TARA wanajivunia idadi ya Wanachama kuongezeka kutoka wanachama 20 kwa mwaka 1976 hadi kufikia wanachama 478 kwa mwaka 2025.

“Ongezeko hili ni kubwa kwetu sisi na linaonyesha jinsi gani wanataaluma wanaona faida za kuwa wanachama. Aidha, ni matamanio yetu kuona idadi ya wanachama ikiongezeka siku kwa siku kwa kuwa wahitimu wa fani hii ni wengi ukilinganisha na idadi ya uanachama wao,”amesema.

Akijibu namna itakavyotatuliwa  changamoto hiyo,Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Cyrus Kiwasuwasu wakati akifungua Mkutano huo wa Mwaka amesema kuwa wameipokea changamoto hiyo watashirikiana na Wizara ya Afya ili kuona namna bora ya kuviwezesha vyuo vinavyota elimu nchini ili kutoa Elimu hiyo kama mlivyopendekeza.

“Nimesikia changamoto yenu ya kutotambulika kwenye nafasi za kibingwa na kibobezi kwenye muundo wa maendeleo ya kiutumishi wa kada ya Radiografa kutokana na kukosekana kwa vyuo hapa nchini vinavyotoa Elimu ya Shahada ya Uzamili wa masuala ya Radiografa niwaahidi tutashughulikia,”amesema Kiwasuwasu.

Pamoja na hayo Kiwasuwasu aliwasihi wanachama wote wa TARA na wataalamu wengine wa Kada za Afya kuzingatia maadili yao na miiko ya kazi kwa kufanya kazi kwa uadilifu na weledi kwa kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Niwasihi kuepuka vikwazo na changamoto kwa wananchi kutokana na huduma zenu mnazozitoa. Epukeni kutoa huduma kwa upendeleo au kwa maslahi binafsi bali mviishi viapo vyenu na kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kuboresha huduma za afya na hasa sehemu ya uchunguzi na matibabu  ya magonjwa kwa njia ya mionzi.

Pia aliwaomba kuwa mabalozi wa kuitangaza nchi yao kwa mazuri na hususan suala la Amani kuendelea kuienzi tunu  walioiacha watangulizi wetu wasikubali kujiingiza kwenye vitendo viovu vinavyoweza kuondoa Amani yetu.

“Nawaomba tuilinde, tuienzi na kuitetea Amani hii,”amesisitiza.

Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi na Vifaa Tiba,kutoka Wizara ya Afya Adam Mrema akizungumza katika Mkutano huo aliwataka wataalam hao kulinda vifaa wanavyovitumia ambavyo ni  Ultrasound mashine, X-ray, MRI, CT Scan na vingene vingi ambavyo vimesambazwa nchi nzima.

“Pamoja na kutoa huduma hizo basi niwaombe mzitunze hizo mali za umma ,mali za serikali pia sisi wenyewe na uwekezaji huu ni wakwetu tuhakikishe zinabadilishwa pale zinapokwisha muda wake lakini pia tuhakikishe  zinatunzwa sehemu sahihi.

“Kwa kutambua nyie ndiyo watu wa kuzishika mashine hizo wa kuziendesha lakini pia kwa kuhudumia wagonjwa,basi kwa moyo huo huo wa kuwahudumia wagonjwa na kutumia vifaa hivyo mvitunze.Lakini pia mhakikishe kuvitunza huku vinatengenezwa kwa wakati,vinatoa huduma kwa wakati lakini kuhakikisha huduma mnzozitoa zinaendelea kufuata miiko na maadili ya kitaaluma.

Mrema amesema kwenye Kongamano hilo pamoja na kukumbushana waliyojifunza  shuleni,lakini pia linawakumbusha uzoefu wanapokuwa katika maeneo yao ya kazi hivyo kujengea chachu na uwezo wa kufanyakazi vizuri zaidi.

Chama cha Wataalam wa Radiografia Tanzania (Tanzania Association of Radiographers) ni chama cha kitaaluma kilianzishwa mwaka 1976 kwa Lengo Kuu la kuwaunganisha pamoja Wataalamu wa Matumizi ya Mionzi (ionizing and non ionizing radiation/Nuclear energy; X-Ray, CT-Scan, Cobalt, LINAC, PET-CT), Mawimbi Sauti (Ultrasound) na Usumaku (Magnetic Resonance Imaging – MRI) katika Uchunguzi na Tiba kwa Magonjwa mbali mbali ili kuwezesha Matibabu Sahihi kwa Wagonjwa. Lengo mahsusi ni kuinua, kuboresha, kutangaza na kusimamia ukuaji wa taaluma yetu hapa nchini na kimataifa.