Na Mwandishi wetu,Timesmajira
TAASISI ya Everlasting Legal Aid Foundation (ELAF) imelaani vikali kauli zenye mwelekeo wa udini zilizojitokeza siku chache baada ya uchaguzi mkuu, ikisema kuwa kauli hizo zinahatarisha misingi ya amani, mshikamano na ustaarabu wa taifa la Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam leo Novemba 23, 2025, Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa ELAF, Dkt. Khamis Masoud, amesema kauli hizo “si tu zimekosa busara, bali pia ni tishio kwa mshikamano wa kitaifa.”
“Udini hauna nafasi katika taifa letu. Umoja wa Watanzania ni mkubwa kuliko tofauti zetu za imani,” alisema
Dkt. Masoud amesema ongezeko la kauli za aina hiyo kunaweza kuleta madhara makubwa kwa jamii, yakiwemo kueneza hofu, kujenga kutokuaminiana, kuchochea ghasia, migawanyiko, na hata kudhoofisha uhalali wa taasisi za umma.
Amebainisha jambo hilo halipaswi kuvumiliwa katika jamii inayojivunia amani kama Tanzania.
Ametoa wito kwa makundi yote ya kijamii kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa nchi yenye mshikamano baada ya uchaguzi, akisisitiza kuwa viongozi wa serikali wanapaswa kuwa makini na kauli zao kwa kuwa ndizo zinazotoa mwelekeo wa taifa.

“Viongozi wa dini wahubiri umoja na siyo chuki, vyama vya siasa vijiepushe kutumia udini kama chombo cha kisiasa, na vijana wasikubali kutumiwa kugawa taifa,” ameongeza Dkt. Masoud.
Aidha, amevitaka vyombo vya habari kuzingatia matumizi ya lugha ya amani na maridhiano katika taarifa na mijadala yao, ili kulinda utulivu wa kitaifa.
Katika hatua nyingine, Dkt. Masoud amependekeza kuanzishwa kwa Majukwaa ya Mazungumzo ya Kitaifa, Tume ya Maridhiano na pia kuimarishwa kwa elimu ya uraia inayojikita katika maadili na misingi ya amani, ili kuendeleza uaminifu wa kijamii na kuijenga Tanzania iliyo na mshikamano wa kweli.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako