Na Angela Mazula
NIMONIA ni miongoni mwa magonjwa yanayotajwa kuchangia idadi kubwa ya vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano.
Unatajwa kuwa ugonjwa hatari unaoambukiza kwa njia ya hewa na kuathiri mapafu ya binadamu ukishambulia zaidi watoto na wazee hapa nchini.
Hata hivyo,tafiti zinaonesha kuwa watoto ndiyo walio katika hatari ya kupoteza maisha kuliko watu wazima kwa sababu ya kinga ndogo mwilini.
Mratibu wa Huduma za Afya Manisapaa ya Ilala Dkt.Willam Sangu anasema kwamba kuna wadudu aina ya bakteria ambao wanathiri mfumo mzima wa hewa na kwenda kuathiri mifuko ya mapafu.
Kwa mtoto kuwa na homa kali na kushindwa kabisa kupumua, kama nimonia imebana zaidi anapata kitu kinaitwa sevia nimonia kwa kupitia kwenye bakteria, na wachache wanapata kwa njia ya virus au hata fangasi, alisema Dkt. Sangu.
Aidha anaeleza Dkt.Sangu, uhusiano mkubwa kwa mtu mwenye Covid 19 na nimonia kwa sababu yote ni magonjwa yanayoambukiza kwa njia ya hewa (air way infection).
“Kwa watoto wenye umri mdogo, mwenye utapiamlo na magonjwa makubwa kama vile maradhi ya moyo, ambao kinga yao imedhoofu na hata pia kwa wazee wenye umri mkubwa au kwa yeyote mwenye kinga dhaifu, wote hawa wapo hatarini kupata maradhi haya ya nimonia’’ anasema.
Anasema “Watoto wanaoishi mjini wako katika hatari kubwa ya kupata magonjwa ya njia hewa kuliko wale wanaoishi vijijini kwa sababu, vijiji hakuna mkusanyiko mkubwa wa watu kama huku mjini kuna mavumbi yanayopatikana kwenye hewa wanayovuta’’.
“Miili ya watoto huwa bado haina kinga ya kutosha kupambana na magonjwa mbalimbali ikiwamo nimonia, ndiyo maana anapougua ikiwa hajapatiwa matibabu sahihi ni rahisi kupoteza maisha,” anabainisha.
Kwa mujibu wa daktari Sangu matibabu ya nimonia yakichelewa na virusi kusambaa mwili hupeleka mtoto akapata maradhi ya uti wa mgongo,figo kuathirika na kuleta shida kwenye moyo.
Ni ugonjwa ambao unaweza kutibika na kuzuilika kwa kujenga kinga ya mtoto kwa lishe bora kwani kinga ya mtoto hupatikana katika kipindi cha miezi sita ya kwanza kupitia maziwa ya mama mpaka mpaka kipindi cha miaka miwili.
Ni muhimu kwa mtoto kupata chanjo zote mpaka miaka mitano hata kama akipata ugonjwa hauwezi kuwa sevia kwa sababu amekamilisha chanjo.
Akizungumzia Manispaa ya Ilala kwa upande wa chanjo Serikali imefanikiwa kuimarisha upatikanaji,uhifadhi na usambazaji wa chanjo, pamoja upatikanaji wa maghala ya kuhifadhia chanjo hizo na ununuzi wa magari 74 ya kubebea chanjo na ununuzi majokofu 1,385 yanayotumia nguvu za jua.
“Wapo pia wazazi na walezi waliojenga utamaduni wa kwenda wenyewe katika maduka ya dawa na kununua dawa za ‘antibiotics’ na kuwapatia watoto wanapopata kikohozi.
Aidha akitoa msisistizo daktari huyo kuwa “Si jambo sahihi, wazazi/ walezi wanatakiwa wajue kwamba si kila kikohozi ni nimonia kitendo cha kuwapatia dawa bila ushauri wa daktari kinaweza kusababisha kutengeneza usugu wa dawa mwilini,”.
Akielezea dalili kuu ya kwanza huwa ni kukohoa au kupumua kwa shida au vyote viwili kwa pamoja, “Yaani unakuta anakohoa au anapumua kwa shida, lakini nisisitize si kila kikohozi ni nimonia, inahitaji uchunguzi wa kina ili uweze kujua kwamba ni nimonia au la kwa sababu matibabu yake yanatofautiana’’.
“Kuna mtoto anaweza kuletwa hospitalini akiwa na tatizo la kikohozi akichunguzwa kasi yake ya upumuaji daktari anakuta haijaongezeka na ipo kawaida kabisa.
“Tafiti zinaonesha pia ugonjwa huo unashika nafasi ya tatu nchini kati ya magonjwa yanayosababisha idadi kubwa ya vifo vya watoto wachanga kutokana na maboresho yaliyofanyika katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano,viashiria vikuu vya mwenendo wa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, vimeendelea kuimarika’’.
Katika magonjwa matano ambayo yanaongoza kwa vifo vya watoto duniani ugonjwa wa kuhara kwa asilimia 9,HIV asilimia 2,ajali kwa asilimia 5, malaria asilima 7 na kwa upande wa nimonia ni asilimia 15.
Katika ngazi ya zahanati Serikali imejengea uwezo mkubwa sana katika utoaji wa elimu kwa watoa huduma namna ya kugundua mapema na katika vituo hivyo vina uwezo mkubwa,chanjo na dawa za kutosha, kliniki maalum za watoto,pamoja kuongeza idadi ya vituo vya Serikali na binafsi.
Kwa mujibu wa taarifa ya huduma za afya kutoka Wizara ya Afya zinaonyesha jumla ya vituo vya kutolea huduma 1,797 vimejengwa (Zahanati 1,198, Vituo vya Afya 487, Hospitali za Halmashauri 99, Hospitali za mikoa 10 ikiwemo Hospitali ya Mkoa wa Mara ya Mwalimu Nyerere Memorial Hospital.
Katika kipindi cha mwaka 2016 -2020 jumla ya Watoa huduma za afya 14,479 wenye ujuzi waliajiriwa na kufikia watumishi 100,631 mwaka 2020 ikilinganishwa na watumishi 86,152 mwaka 2015 pamoja na madaktari, wauguzi na wakunga, wafamasia, wataalamu wa maabara.
Naye daktari Mswela Kanyaki anasema wapo watu ambao huamini kwamba kitendo cha mtu kuishi katika maeneo yenye baridi kali moja kwa moja humuweka kwenye hatari ya kupata ugonjwa huo lakini si kweli.
“Ingawa kuna baadhi ya tafiti (sayansi) ambazo inaonesha mazingira ya baridi ni hatarishi kwani wale wadudu wanaweza kuzaliana kwa wingi lakini si sababu ya msingi mno kwamba watu wanaoishi katika maeneo hayo huathirika zaidi kuliko maeneo mengine.
“Watoto wakiwekwa katika mazingira ya moshi, yaani unakuta watu wanapikia ndani na kuna moshi labda unaotokana na kuni, mkaa au sigara, moja kwa moja mtoto huwa kwenye hatari ya kupata tatizo hili la ugonjwa wa nimonia’’.
“Lishe ni jambo la muhimu pia katika kumkinda mtoto kupata tatizo hili hasa inayotokana na maziwa ya mama humuepusha mtoto dhidi ya ugonjwa huu,” anabainisha.
Anasema licha ya changamoto iliyopo kwa baadhi ya wazazi na walezi kutowafikisha watoto wao mapema hospitalini kwa ajili ya kupatiwa matibabu, serikali imeendelea kujitahidi kuwapatia chanjo wale wanaofikishwa hospitalini kuwakinga dhidi ya ugonjwa huo.
“Matokeo ya Utafiti wa ‘Global Action Plan for Nimonia’ uliotolewa mapema mwaka huu ambapo takriban nchi 20 tulifanyiwa ufuatiliaji, Tanzania imeongoza kwa asilimia 90 katika utoaji chanjo dhidi ya nimonia,” anabainisha.
Anasema huduma hiyo inatolewa nchi nzima hasa katika vituo vyote vinavyotoa huduma ya mama na mtoto.
Anasema licha ya matokeo haya yaliyoonesha mafanikio,bado tunahitaji kuihamasisha jamii kuhakikisha watoto wanafikishwa mapema hospitalini ili kufikia kiwango cha asilimia 100.
“Ni muhimu mtoto afanyiwe uchunguzi, nasisitiza kwamba si kila kikohozi ni nimonia inahitaji uchunguzi kujua kwa sababu matibabu yake yanatofautiana na ikiwa atapatiwa dawa kiholela ni hatari zaidi,” anasema.
More Stories
Hivi ndivyo TASAF ilivyoshiriki kumaliza kilio cha wananchi Kata Bwawani, Arusha
Mfumo unavyokwamisha wanawake kuwa viongozi
Mussa: Natamani kuendelea na masomo,nikipata shule ya bweni