Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online -Mwanza
Washtakiwa 93 wa kesi za uharibifu wa mali, kufanya vurugu na unyang’anyi wa kutumia silaha Novemba 19,2025,wamefikishwa tena katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana, Mwanza, huku upande wa Jamhuri ukitakiwa kukamilisha ushahidi haraka katika kosa la kwanza la uharibifu wa mali.
Katika shauri hilo la jinai namba 26546 la mwaka huu, washtakiwa hao 93 wanadaiwa kutenda makosa hayo kinyume na kifungu cha 326 (1) cha Sheria ya kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Marejeo ya mwaka 2023 kwa kosa la kwanza na kifungu cha 287 A cha Sheria hiyo.
Washtakiwa hao ni kati ya 172 walikamatwa na Jeshi la Polisi na kufunguliwa mashtaka mbalimbali Wilayani Nyamagana kufuatia matukio ya vurugu yaliyotokea kati ya Oktoba 29 na 31, mwaka huu.
Shauri hili limetajwa kwa mara ya pili Novemba 19, 2025, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Amani Sumari, baada ya kutajwa kwa mara ya kwanza Novemba 7, mwaka huu.
Kesi hiyo iliambatana na umati wa watu nje ya viunga vya mahakama hiyo, wakitarajia kuona ndugu zao wakiachiwa, wakiongozwa na agizo la hivi karibuni la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuvitaka vyombo vya dola kuchuja washtakiwa hao na kuwaachia wale waliofuata mkumbo.
Katika Mahakama, upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Mawakili wa Serikali, Tunu Msangi na Prince Masawe, huku utetezi ukiwakilishwa na Mawakili kutoka Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Duttu Chebwa na Beatus Linda.
Mwanzo wa shauri hili, Wakili wa Serikali, Tunu Msangi, aliwasilisha ombi la kubadilisha hati ya mashtaka ili kuongeza washtakiwa wengine sita (6) ambao hawakuwa wamejumuishwa hapo awali.
Pia aliomba muda wa siku 90 wa kufanya upelelezi zaidi, akisisitiza kuwa upelelezi wa mashtaka yote mawili bado haujakamilika.
Upande wa utetezi, ukiongozwa na Wakili Duttu Chebwa, ulipinga vikali hoja ya kuongeza muda wa upelelezi, ukihoji kwa nini upelelezi unachukua muda mrefu katika kosa la kwanza la kuharibu mali.
Chebwa alisisitiza kuwa hati ya mashtaka inaeleza wazi mali zilizoharibiwa na maeneo husika na hivyo wanashangazwa ni maelezo gani zaidi yanahitajika kukamilisha ushahidi.
Akijibu hoja hiyo, Wakili Msangi alisisitiza kuwa wanahitaji muda zaidi kwa kosa la pili ili waweze kupata tathmini ya mali na vitu vilivyoharibiwa.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Sumari amekubali ombi la upande wa Jamhuri la kufanya marekebisho kwenye hati ya mashtaka.
Hata hivyo, ameiagiza Jamhuri kukamilisha ushahidi wa kosa la kwanza (Kuharibu mali) haraka, akitaka warekebishe makosa kwenye hati ya mashtaka ambayo ilitaja Halmashauri ya Nyamagana, badala ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambayo ndiyo inayotambulika kisheria.
Hakimu Sumari amehairisha shauri hilo hadi Desemba 2, 2025 Saa 3:30 asubuhi kwa ajili ya kutajwa tena.
Pia hakimu huyo amekubali kuwa kosa la pili ni kubwa hivyo linahitaji muda zaidi kukamilisha upelelezi wake.
Baada ya maelezo hayo, ya Hakimu Sumari, washtakiwa wamerejeshwa rumande hadi tarehe iliyopangwa.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi