Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mwanza, Mhashamu Renatus Nkwande, amesema kilichotokea wakati na baada ya uchaguzi nchini mwaka huu ni fedhea na kinalishushia heshima taifa iliyojengeka kwa miaka mingi pamoja na kutia kasoro ambayo inapaswa kulaaniwa,kuisemea na kuikemea.
Amesisitiza kuwa kama kweli Taifa linahitaji kutatua tatizo ni vyema warudi kwenye meza ya mazungumzo huku akisisitiza umuhimu wa kukiri na kutubu.
Askofu Nkwande amesisitiza kuwa taifa lisipokuwa tayari kukiri na kutubu, haliwezi kupata tiba ya tatizo lililosababisha maafa hayo.
Amesema njia pekee ya kufikia suluhu ya kudumu ni kurejea kwenye meza ya mazungumzo na kukubaliana kama taifa kuhusu mustakabali wa haki, amani na maridhiano.
Askofu Nkwande,amezungumza hayo Novemba 13,2025 katika adhimisho la misa takatifu ya Jimbo Kuu la Mwanza la kuombea marehemu walipoteza maisha wakati na baada ya uchaguzi,iliofanyika Kanisa Kuu la Epifania Bugando jijini Mwanza.
Ambapo ametoa wito kwa Watanzania kurejea katika toba,mazungumzo na misingi ya utu ili kuponya majeraha yaliyosababishwa na maandamano yaliozaa kuvurugu wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 uliofanyika Oktoba 29,2025,zilizotokea nchini kwa baadhi ya mikoa ikiwemo Dar-es-Salaam,Mwanza,Mbeya na Arusha.
“Tusikimbie ukweli,turejee meza ya mazungumzo,akinuuku baadhi ya vifungu kutoka Zaburi 15,Injili ya Mathayo na Luka.Poleni Watanzania, hili liwe fundisho na kamwe lisijirudie, na kama kweli tunataka kumaliza turejee meza ya mazungumzo, na walioshiriki wakiri dhambi zao,” amesema Askofu Nkwande.
Pia ametoa pole kwa waathirika wa vurugu hizo na Watanzania kwa ujumla akisema msiba huo ni wa Taifa,ambapo amesema wapo waliofikwa na umati katika harakati za kuonesha hisia zao hivyo walipaswa kusikiliza.
“Lakini wapo waliofariki wakiwa nyumbani,wanaotoka hospitali na waliokuwa wanakimbia ovyo kwa sababu Watanzania hawajazoea kusikia milio ya risasi.Inatupasa kuwakumbuka ndugu na familia za waliopoteza watu wao kwenye matukio hayo, kwa kuwatembelea, kuwapa pole, kuwafariji na kuwapa moyo,”amesema Askofu Nkwande na kuongeza:
Kwa upande wake mmoja wa waumini waliohudhuria misa hiyo,Liberatus Ndegeulaya,amesema katika hali ya kawaida binadamu wanapokuwa wamekinzana suluhu pekee ya uhakika ya kupata kile kinachohitajiwa ni katika meza ya mazungumzo.
Amani haiwezi kupatikana kama hakuna meza ya mazungumzo hivyo amesisitiza pande zinazokinzana kurudi mezani na kutazama wapi wamekosea na kuanguka hili yaliojitikeza kwenye nchi yasijirudie tena.
“Kwenye neno la Baba Askofu tunapata ujumbe zaidi kwamba tunatakiwa kutanguliza utu.Utu ndio hasa kiini kinachoweza kutufanya tukabaki na amani lakini amani haiji hivi hivi,amani imejengwa katika misingi ya haki,”amesema Ndegeulaya na kuongeza kuwa:
“Baba Askofu ametuhasa tuzidi kusisitiza haki ili amani iweze kufika kwa watu wote,na katika Zaburi aliotupishisha anasisitiza misingi ya hayo yote ya imani yetu inajengwa katika haki na katika haki tunapata amani,”.
Naye Joyce Anthony,amesema Askofu huyo amewagusa mioyo yao baada ya matukio hayo yalioleta mshtukio hivyo wanapaswa kupendana na kuleta amani katika nchi.
“Naomba viongozi waliopo madarakani washikamane wawe na amani na upendo ili waweze kuongoza taifa letu,”.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako