March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkalipa asisitiza ushiriki wa wazazi lishe shuleni

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza 

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza,AmirI Mkalipa amesisitiza juu ya kufanyika kwa vikao vya wazazi ili kuwahamasisha na kuwahimiza kuchangia chakula shuleni kwa ajili ya watoto wao.

Mkalipa ametoa rai hiyo wakati akiongoza kikao cha tathmini ya lishe Wilaya,Novemba 13, 2025,kilichofanyika kwa ajili ya kujadili taarifa ya Julai – Septemba 2025/26.

Ambapo amewataka Watendaji wa Kata kuhakikisha Maofisa Ugani Kilimo kwa kila kata wanasimamia mashamba na bustani katika shule ambazo zina maeneo kwa ajili ya kilimo ili kuwezesha upatikanaji wa chakula shuleni.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za lishe kwa kipindi cha Julai – Septemba 2025/26,Ofisa Lishe wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Pili Kassim,amesema kuwa kiasi cha shilingi milioni 30 zilitumika kutekeleza shughuli za lishe.

Ambapo jumla ya shughuli 12 zimetekelezwa ikiwemo mafunzo kazini kwa watoa huduma 28, maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji pamoja na shughuli zingine.

Kwa upande wake Mkaguzi wa chakula,Francis Dougan,amesema kuwa kati ya mafanikio waliyoyapata ni pamoja na kuzifikia shule 38 na wauza vyakula 268 ambao waliwapatia elimu ya usalama wa chakula.

Wakijadili taarifa ya ukaguzi wa chakula, wajumbe walishauri kuendelea kutolewa elimu kwa wananchi ya  namna bora ya kuepukana na magonjwa ya mlipuko.