March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nkasi yakabidhi pikipiki kwa maofisa maendeleo ya jamii Kata za Kizumbi na Ninde

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online -Rukwa

Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa imekabidhi pikipiki mbili kwa Maofisa Maendeleo ya Jamii ngazi ya kata, kwa lengo la kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.

Akikabidhi pikipiki hizo kwa Maofisa Maendeleo ya Jamii wa Kata za Kizumbi na Ninde, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Valeriana Mwampasi, amewataka Maofisa hao kuzitunza vyema na kuhakikisha zinatumika kwa matumizi sahihi ili ziweze kutoa huduma endelevu kwa wananchi wanaoishi katika maeneo hayo.

Mwampasi amesema kuwa lengo la Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalum kutoa pikipiki hizo ni kuhakikisha jamii inafikiwa kwa haraka na kwa uhakika, hivyo ni muhimu kwa watumishi hao kuhakikisha pikipiki hizo zinatunzwa vizuri na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Awali,Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Nkasi, Lucy Mhina,amesema kuwa Kata za Kizumbi na Ninde ni miongoni mwa maeneo yenye changamoto za kijiografia, hali inayowafanya Maofisa Maendeleo ya Jamii kukabiliwa na ugumu wa kuwafikia wananchi kwa urahisi.


Amesema kupatiwa pikipiki hizo kutarahisisha kazi zao na kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi wengi zaidi.

Mhina amewataka Maofisa hao kuonesha matokeo chanya kufuatia kukabidhiwa pikipiki hizo, kwani Serikali ina imani nao katika kuhakikisha huduma za kijamii zinawafikia wananchi wote.

Kwa upande wao, Maofisa Maendeleo ya Jamii wa Kata za Kizumbi na Ninde, Credo Khamis na Henry Khamis, wameishukuru Serikali kwa kuwapatia pikipiki hizo, wakibainisha kuwa zitawasaidia kutokana na ugumu wa mazingira na changamoto za kijiografia zilizopo katika kata zao.