*Yasisitiza kumzawadia Dkt. Samia kura milioni 4.6 za “Asante”
Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online – Mwanza
Katibu Mkuu wa Taifa wa Umoja wa Vijana wa Sekta ya Madini Tanzania (TYM), Ashraph Omary, amewataka vijana wachimbaji madini nchini kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 huku akiwasisitiza kuepuka maandamano yanayoweza kuchochea vurugu.
Omary amezungumza hayo, Oktoba 27,2025 na waandishi wa habari jijini Mwanza,ambapo amesema vijana wanapaswa kuepuka kushiriki katika maandamano yasiyo na tija ambayo yanaweza kusababisha vurugu na kuathiri biashara ya madini nchini.

“Biashara ya madini duniani haiwezi kufanyika kwenye nchi isiyo na amani. Nchi jirani zenye misukosuko ya vita hulazimika kupitisha dhahabu zao nchini Tanzania ili zipate kibali cha soko la dunia. Tusiingie kwenye machafuko yatakayoporomosha dhahabu yetu,” amesema Omary.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TYM Mkoa wa Mwanza, Cuthberth Joseph,amesema umoja huo umeazimia kuendelea kushirikiana na Serikali katika kukuza sekta ya madini ili vijana waendelee kunufaika kiuchumi, huku ikiahidi kumpa Dkt. Samia kura milioni 4.625 kama “asante” kwa mchango wake katika kuwawezesha vijana.
Amesema, kura hizo ni zawadi ya shukrani kwa Dkt. Samia kutokana na namna alivyowainua vijana wachimbaji tangu alipoingia madarakani mwaka 2021.
“Tulipoanza tulikuwa na wanachama 600,000 pekee, sasa tupo 4,681,000.Kati yao, 4,625,000 wamejiandikisha kupiga kura na wote wameahidi kumpigia kura Dkt. Samia kama ishara ya kumshukuru,” amesema Joseph.
Alibainisha kuwa baada ya kuanzishwa kwa umoja huo, Serikali iliwatambua rasmi kwa kuwapa cheti cha usajili, leseni 11 za uchimbaji pamoja na leseni kubwa ya utafiti wa madini.
“Dkt. Samia alitupatia mitambo miwili ya kuchorongea yenye thamani ya bilioni 36, na ametuwekea gharama nafuu ya kuchoronga mita moja kwa sh 200,000 badala ya dola 250 ambazo tulizokuwa tunatozwa na kampuni za kigeni,”amesema Joseph.
Joseph amesema,kupitia maelekezo ya Dkt. Samia kwa Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, vijana wapatao 2,000 wanaozunguka mgodi wa Nyamongo wamepatiwa leseni za uchimbaji, jambo lililosaidia kupunguza kuvurugu zilizokuwa zinatokea kwa sababu ya ukosefu wa ajira.
Pia amesema,Dkt.Samia ameanzisha mradi wa Mining for Brighter Tomorrow (MBT) unaolenga kuwawezesha vijana wachimbaji zaidi ya milioni 4, pamoja na kuimarisha mfumo wa manunuzi ya dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kusaidia taifa kuwa na akiba ya dhahabu.
“Sasa dhahabu inanunuliwa kwa bei ya soko la dunia, ambapo gramu moja inauzwa kwa zaidi Sh 300,000 na malipo hufanyika papo kwa hapo. Hii imeleta tija kubwa kwa wachimbaji na taifa kwa ujumla,”amesema Joseph.


More Stories
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10