March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yafikisha siku 60 za kampeni za Urais

*Kihongosi atoa mrejesho wa mafanikio,ataja afya na nguvu za Dkt.Samia kuwa imara

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online Mwanza

Katibu wa NEC  Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi(CCM),Kenan  Kihongosi, amesema kampeni za chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 29 2025 zimefanyika kwa mafanikio makubwa.

Huku mgombea wa kiti cha urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiendelea kuwa na afya njema na nguvu kubwa baada ya kufanya mikutano 112 katika kipindi cha siku 60.

Akizungumza jijini Mwanza Oktoba 27,mwaka huu  Kihongosi,amesema kampeni hizo, ambazo zilianza Agosti 28, 2025 katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar-es-Salaam, zinatarajiwa kufikia tamati  Oktoba 28, 2025, kwenye uwanja wa CCM Kirumba mkoani hapa.

“Leo tunakutana kutoa mrejesho wa safari yetu ya kampeni za urais. Tumezunguka nchi nzima, tumewasikiliza wananchi, tumewajengea matumaini mapya kupitia Ilani ya CCM ya uchaguzi mkuu 2025,”amesema Kihongosi.

Kihongosi amesema katika kipindi cha kampeni,takribani watu milioni 25.3 wamehudhuria mikutano ya hadhara ya chama hicho kwa nafasi ya mgombea Urais huku watu milioni 57.1 wamefuatilia kampeni kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Takwimu za kidijitali zinaonesha kampeni za Dkt. Samia kufuatiliwa mara milioni 164.9 kupitia majukwaa mbalimbali ya mtandaoni.

“Wingi wa watu waliomfuatilia Dkt. Samia ni ishara ya imani kubwa kwa Chama Cha Mapinduzi na upendo wa wananchi kwa uongozi wake wa kuzingatia utu na matokeo halisi,”amesema Kihongosi.

Pia amesema Ilani ya CCM ya mwaka 2025 ni ya kipekee kwa sababu inagusa maeneo yote ya maisha ya Watanzania na inatoa mwanga wa ajira, afya bora, na ustawi wa jamii.

Inaweka msingi wa gridi ya maji ya taifa na uzalishaji wa umeme wa zaidi ya megawati 8,000,inahamasisha mapinduzi ya kilimo, ufugaji wa kisasa, na uchumi wa viwanda.

Pamoja na kutoa nafasi kubwa kwa sekta binafsi na inalenga kuongeza thamani ya rasilimali kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa.

“Afya ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ni njema kabisa. Amezuru kila kona ya nchi, kuzungumza na Watanzania anaowapenda. Tupo salama, tumefanikiwa, na tumeshuhudia ulinzi bora katika kila hatua ya kampeni,”amesema Kihongosi.

Sanjari na hayo ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, 2025, na kuhakikisha wanaweka alama ya tiki kwa wagombea wa CCM.

“Kitendo cha kupiga kura ndicho kinachokuthibitisha kuwa raia unayetambua haki na wajibu wako. Tumpigie kura Dkt. Samia Suluhu Hassan na wagombea wote wa CCM,” amesema Kihongosi.

Hata hivyo ametoa wito  kwa wananchi kuhudhuria mkutano wa funga kazi wa kampeni utakaofanyika Oktoba 28, 2025, uwanja wa CCM Kirumba au kufuatilia kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.