*Asisitiza uzingatiwaji wa sheria, kanuni, miongozo wakati wa uchaguzi
*Wasimamizi, wasimamizi wasaidizi wa vituo 2870 wapatiwa mafunzo
*Vituo 944 kutumika kupigia kura Ilemela
Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza,wametakiwa kutokuwa chanzo cha malalamiko na vurugu na badala yake wazingatie katiba,sheria,kanuni na maelekezo hadi watakapokamilisha zoezi la uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29,2025.
Huku wakisisitizwa kuzingatia uzalendo na umakini katika kutekeleza jukumu hilo la kitaifa.
Hayo yamezungumzwa Oktoba 26,2025 na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ilemela Herbert Bilia,wakati akifungua mafunzo muhimu ya siku mbili kwa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu mwaka huu.

Ambapo amesema mafunzo hayo yamegawanyika katika makundi matano,ambapo kwa kundi ambalo limejumuisha Kata ya Kitangiri,Kirumba,Kawekamo na Nyamanoro,yamefanyika Rock City Mall ambapo jumla ya washiriki ni 690.
Bilia amesema,uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kikatiba na kisheria, ambazo hupaswa kufuata na kuzingatiwa hasa katika ngazi ya kituo.
Ambapo mchakato wa kupiga kura na kuhesabu kura huendeshwa na hatimaye matokeo ya uchaguzi kwa kiti cha Rais, Ubunge na Udiwani ndio yanapoanzia.
“Hatua na taratibu hizo ndio msingi wa uchaguzi huru na wa haki na hatimaye kupunguza na kuondoa kabisa malalamiko au vurugu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi,hivyo nawaasa msiache kufuata na kusoma katiba,kanuni, taratibu, miongozo na maelekezo yanayotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi(INEC),”amesema Bilia.
Hivyo amewasisitiza kujitahidi na kujiepusha kuwa vyanzo vya malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa kwa kushirikiana vyema na mawakala wa vyama hivyo watakaokuwepo vituoni kwa mujibu wa sheria.
“Zingatie unadhifu,lugha nzuri na kutoa kipaumbele kwa wapiga kura wenye mahitaji maalumu watakapofika kituoni,”amesema Bilia.
Sanjari na hayo Bilia,amesema Jimbo Zima la Ilemela lina jumla ya wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura 2870, vituo 994 kwa Kata ze 19 za Jimbo la Ilemela.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mafunzo hayo,Frezynery Manyonyi,amesema,wanatarajiwa kufanya jukumu hilo vyema huku akisisitiza kuhakikisha wanasoma na kuzingatia, miongozo,katiba,sheria na maelekezo ili kuepuka kusababisha migogoro.
Mkufunzi wa mafunzo hayo,Isaya Hosea,amesema mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura,ili Oktoba 29,mwaka huu waweze kutekeleza majukumu yao vizuri,hivyo amewahimiza wananchi kujitokeza siku hiyo ya kupiga kura.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo,akiwemo Emmanuel Charles,amesema wamejipanga kuzingatia uzalendo, uadilifu na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria hili kuhakikisha wanahudumia wananchi na kukamilisha zoezi la uchaguzi kwa amani.
“Kulingana na mafunzo haya mimi na wenzangu tutahakikisha tunafanya kazi kwa uzalendo na kuepuka changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza wakati wa uchaguzi na kuchelewesha matokeo ya uchaguzi.Hivyo tutajitoa kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia makundi yote ikiwemo ya mahitaji maalumu kama walemavu,wazee na wengine kupata haki pasipo upendeleo,”amesema Charles.
Zainabu Shija,amesema,atasimamia uchaguzi vizuri na kuhakikisha anatenda haki na kutekeleza jukumu la alilopewa kwa mujibu wa sheria.


More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako