March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi wahimizwa kujitokeza kupiga kura ,Dodoma ipo salama

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

WANANCHI wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, huku wakidumisha amani na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ambaye amesisitiza kuwa Mkoa wa Dodoma uko salama na serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Akizungumza Oktoba 24, 2025, katika kikao na waandishi wa habari mkoani Dodoma kilicholenga kujadili maendeleo ya mkoa na maandalizi kuelekea uchaguzi, Senyamule amesema ni wajibu wa kila Mtanzania kutumia haki yake ya kikatiba ya kupiga kura kwa utulivu na bila hofu.

 “Natoa wito kwa wananchi wote wa Dodoma kujitokeza kwa wingi kupiga kura. Mkoa wetu upo salama, na serikali imejipanga kuhakikisha kila eneo linakuwa salama wakati wa uchaguzi,” amesema Senyamule.

Aidha, ameviasa vyombo vya habari kutumia taaluma yao kuwahamasisha wananchi kushiriki uchaguzi, kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kupiga kura na kuendelea kuhimiza amani katika kipindi chote cha uchaguzi.

 “Vyombo vya habari vina nafasi muhimu sana katika kipindi hiki. Tusaidieni kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kushiriki uchaguzi na kudumisha amani kwa ajili ya maendeleo ya mkoa wetu na taifa kwa ujumla,” ameongeza.

Mkuu huyo wa mkoa amebainisha kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, idadi ya wapiga kura waliojitokeza mkoani Dodoma ilikuwa chini, hivyo mwaka huu serikali na wadau wamejipanga kuongeza mwamko wa wananchi kushiriki katika uchaguzi Mkuu kwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

 “Tumeweka ajenda ya kitaifa ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu. Tunataka kuona kila mwananchi anashiriki kikamilifu katika kuamua mustakabali wa nchi,” alisema.

Mkutano huo ulihudhuriwa na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali, baadhi ya viongozi wa taasisi zaserikali, waliokuwa wakijadili mafanikio ya maendeleo ya Mkoa wa Dodoma katika kipindi cha miaka minne iliyopita pamoja na maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.