
Na Joyce Kasiki ,Timesmajira online,Mbeya
rikali chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaendelea kutekeleza mikakati ya kuhakikisha vijana wanapata fursa sawa za kujiletea maendeleo binafsi na kuchangia katika ustawi wa Taifa kwa ujumla.
Mikakati hiyo inajumuisha uanzishaji wa mifumo ya kitaasisi, kisera, mipango kazi, miongozo na sheria zinazolenga kutatua changamoto zinazowakabili vijana katika nyanja tofauti za kijamii na kiuchumi.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bi. Mary Maganga, wakati wa ufunguzi wa kongamano la siku mbili la Vijana Tanzania, linalofanyika kuanzia leo, 12 Oktoba hadi 13 Oktoba, 2025 jijini Mbeya katika Ukumbi wa City Park Garden.

Bi. Mary Maganga amesema lengo la kongamano hilo ni kuwajengea vijana ujuzi na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika mabadiliko ya kijamii na kiuchumi, kukuza ushirikiano na ubadilishanaji wa mawazo, pamoja na kutambua na kuunga mkono mipango na miradi ya vijana inayolenga kuinua uchumi wao.
“Vijana ni nguvu ya mabadiliko na maendeleo katika jamii zetu. Ni lazima tutumie vyema nguvu hii kubadilisha dunia kuwa mahali bora kwa ajili ya wote,” amesema Katibu Mkuu huyo.
Aidha, amewataka vijana kutumia kongamano hilo kama fursa ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto zinazowakabili, ili Serikali iweze kuyachukua maoni yao na kuyatumia kuboresha sera, sheria, kanuni na miongozo kwa manufaa ya vijana wote nchini.
Sambamba na hilo, Bi. Mary amewahimiza vijana kote nchini kujitokeza kushiriki katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, kwa kuchagua viongozi wanaoakisi matumaini, malengo na ndoto za taifa hili.
Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Rodrick Mpogolo, aliwasihi vijana kuendelea kuipenda nchi na kujivunia Taifa la Tanzania kwa kuwa ni mahali ambapo kila kijana ana mchango wa kuleta maendeleo.
Akizungumza kuhusu idadi ya washiriki wa kongamano hilo, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Seleman Mvunye, alisema limehusisha zaidi ya vijana 1,500 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, pamoja na Maafisa Vijana kutoka Halmashauri zote nchini.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina