March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nitahakikisha kila aliyedhulumiwa anarudishiwa haki yake Othman Masoud

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, ameahidi kurejesha haki za wananchi wote waliodhulumiwa mali au ardhi zao pindi atakapoingia madarakani.

Akizungumza na wauza madagaa katika eneo la Fungu Refu, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Othman alisema moja ya changamoto kubwa inayowakabili wananchi ni kunyimwa haki zao kutokana na mifumo dhaifu ya utawala na upendeleo unaojitokeza katika taasisi za umma.

“Serikali ya ACT Wazalendo haitakuwa ya maneno matupu. Tutasimamia haki za wananchi wote, na kila aliyeonewa atarejeshewa stahiki zake kwa mujibu wa sheria,” amesema Othman.

Mgombea huyo ametumia fursa hiyo kusikiliza kero na changamoto za wafanyabiashara hao wadogo, ikiwamo ukosefu wa masoko, miundombinu duni na vikwazo katika utoaji wa leseni, akiahidi kuweka mazingira bora zaidi ya biashara visiwani humo.

Amesema serikali anayoitarajia kuunda itatoa kipaumbele kwa wafanyabiashara wadogo ili waweze kuchangia ipasavyo katika kukuza uchumi wa Zanzibar.

“Wafanyabiashara wadogo ni uti wa mgongo wa uchumi wetu. Tukiwapa nguvu na haki, tutakuwa tumewainua wananchi wote,” ameongeza.