Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Mbeya
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa leo amefungua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa mkoani Mbeya huku akieleza dhamira ya Serikali katika kuwakwamua vijana udiwani pamoja na kuanzishwa Programu ya Uanagenzi iliyo chini ya ofisi yake.
Akizungumza leo Oktoba 10,2025 wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo ,Waziri Mkuu Majaliwa amesema Programu hiyo inalenga kuwapa vijana ujuzi wa vitendo bila kujali kiwango chao cha elimu .
Amesema, kupitia mpango huo, vijana hupelekwa kwenye vyuo maalumu kwa mafunzo ya muda wa miezi sita, ambapo serikali hulipia ada zote.
“Vijana hawa hufundishwa ujuzi mbalimbali unaochochea biashara na uwekezaji kama vile ufundi wa magari, umeme, uchomeleaji, usindikaji na ufungashaji wa vyakula, ushonaji, ususi na urembo pamoja na matumizi ya kompyuta. Lengo ni kuwawezesha kuingia moja kwa moja katika soko la ajira au kujiajiri,” ameeleza Waziri Mkuu.
Ameongeza kuwa tangu kuanzishwa kwa programu hiyo mwaka 2022 hadi sasa, zaidi ya vijana 77,228 wamenufaika kwa kupata mafunzo katika vyuo mbalimbali nchini.
Waziri Mkuu Majaliwa amewahimiza vijana kote nchini kutumia fursa zilizopo za mafunzo na uwezeshaji ili kujikwamua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Aidha amesema ,maadhimisho hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Siku ya Vijana Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kutambua mchango wa vijana katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa, sambamba na kuwapa nafasi ya kujadili mafanikio, changamoto na mustakabali wao katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).
Amesema serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha vijana wanapata elimu, maarifa, na ujuzi utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa nchi.
Kuhusu mikakati iliyopo nchini kwa ajili ya vijana amesema, serikali imefanya maboresho ya Sera ya Maendeleo ya Vijana kutoka toleo la mwaka 2017 hadi sasa sera mpya ya mwaka 2024, ambayo imezingatia mahitaji halisi ya vijana wa Kitanzania. Sera hiyo inalenga kuimarisha maendeleo ya vijana kupitia ushirikiano wa karibu kati ya serikali, vijana wenyewe, na wadau wa maendeleo.
Aidha, amebainisha kuwa serikali imeendelea kuimarisha Programu ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, ambapo huduma na taarifa muhimu juu ya namna ya kupata mitaji na ujuzi hutolewa kupitia mifumo mbalimbali ya serikali.
Katika kuboresha elimu kwa vijana, Mheshimiwa Majaliwa amesema serikali inaendelea kutoa elimu bila ada kwa ngazi ya msingi na sekondari, huku wanafunzi wa elimu ya juu na elimu ya kati wakinufaika na mikopo ya elimu. Vilevile, serikali imeimarisha vyuo vya ufundi stadi ili kuhakikisha vijana wanapata ujuzi wa moja kwa moja utakaowawezesha kuajiriwa au kujiajiri.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amewahamasisha vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
“Ni wajibu wenu vijana kuhakikisha mnapiga kura kuchagua viongozi wenye maono, wanaojali maslahi ya vijana, na watakaowaletea maendeleo endelevu. Msikilize kila mgombea anachowaahidi, kisha mfanye uamuzi wa busara,” amesema.
Amesisitiza kuwa vijana wa Tanzania ni wasomi na waelewa, hivyo wana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi yatakayochochea maendeleo ya taifa.
Aidha, aliwasihi vijana kuendelea kushirikiana, kujadiliana na kutoa maazimio yatakayosaidia serikali kuboresha mipango ya maendeleo kwa vijana, na kuhakikisha kila fursa inayotolewa na serikali inawafikia vijana wote kwa usawa.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete, alieleza kuwa maadhimisho haya hutoa jukwaa la kukutanisha wadau wa maendeleo kwa ajili ya kutathmini na kuenzi mchango wa vijana.
Aidha, aliwakumbusha vijana mchango mkubwa uliotolewa na waasisi wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, ambao wakati wa harakati za ukombozi wa Taifa na Afrika kwa ujumla walikuwa bado vijana.
Aliwataka vijana wa sasa kuiga mfano wa kujituma, uzalendo, na moyo wa kujitolea katika kuijenga Tanzania mpya.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina