


Na Joyce Kasiki – TimesMajira Online, Geita
MKUU wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, ametoa wito kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Bodi ya Bima ya Amana (DIB) kuongeza kasi ya kuwafikia wananchi wanaoweka akiba zao kwenye vikundi vidogo vya kifedha kama vile SACCOS na VICOBA, ili kuhakikisha usalama wa mitaji ya Watanzania.
Komba ametoa rai hiyo leo Septemba 26,2025 alipotembelea banda la DIB katika maonyesho ya nane ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, akieleza kuwa bado wapo wananchi wengi wanawekeza kwenye taasisi zisizosajiliwa, jambo linalowaweka kwenye hatari ya kupoteza fedha zao.
“Inawezekana Watanzania wanawekeza sehemu ambazo bado hazijasajiliwa. Nitoe ushauri kwamba Bodi ya Bima ya Amana iendelee kujikumbusha kuwa mdau muhimu ni Benki Kuu. Wanatakiwa kushuka chini kwa kasi kubwa kuwafikia SACCOS na VICOBA ili kuhakikisha mitaji ya wananchi inabaki salama,” amesema Komba.
Ameeleza kuwa katika ofisi yake, wamepokea malalamiko kutoka kwa wananchi waliopoteza fedha zao walizowekeza kwenye vikundi vya kifedha visivyo rasmi, akitoa mfano wa mtu aliyepoteza kiasi cha shilingi milioni 30 baada ya uwekezaji wake kuteketea.
“Unampokea mwananchi anakwambia nimewekeza hisa hadi milioni 30, lakini zote zimepotea,tunaanza kuhangaika kutafuta aliyekuwa kiongozi wa kikundi,hili ni tatizo kubwa linalohitaji ufuatiliaji wa karibu na hatua za haraka,” ameongeza.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano wa DIB Lwaga Mwambande ambaye ni mwakilishi wa DIB katika maonyesho hayo, amepokea ushauri huo na kuahidi kuendelea kushirikiana na wadau wengine wa sekta ya fedha ili kuhakikisha usalama na uaminifu wa mifumo ya kifedha nchini.
“Tutaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, si kwa lengo tu la kuwarudishia wananchi fidia ya pesa zao iwapo benki itashindwa, bali pia kujenga imani kwa wananchi katika mfumo rasmi wa fedha,” amesema Mwambande.
Mwambande amefafanua kuwa kwa sasa, kinga inayotolewa na DIB kwa wananchi wenye amana kwenye taasisi rasmi za kifedha ni hadi kiwango cha shilingi milioni 7.5, kiwango ambacho kinatosheleza kuwalinda asilimia 99 ya wananchi wenye amana katika benki.
“Kinga hii inamaanisha kuwa, endapo benki itafungwa au kushindwa kuendelea na huduma, wananchi wenye akiba hadi milioni 7.5 wana hakika ya kurejeshewa fedha zao kwa haraka,” amesema.
Aidha, Mwambande amesisitiza kuwa kinga hii inalenga si tu kulinda rasilimali za wananchi, bali pia kuendeleza ustawi wa uchumi wa Taifa kwa kuhamasisha wananchi kuwa na imani na kuendelea kutumia mifumo rasmi ya kifedha.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina