March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Geita atoa rai kwa wananchi kuepuka Taasisi za Kifedha zisizosajiliwa

Na Joyce Kasiki – Timesmajira Online, Geita

MKUU wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, ametoa rai kwa wananchi kuepuka taasisi za kifedha zisizosajiliwa na kusisitiza umuhimu wa kutumia taasisi rasmi zinazotambuliwa na serikali ili kuepuka hasara, manung’uniko, na mikopo umiza na  yenye masharti kandamizi.

Akizungumza leo Septemba 26,2025 katika maonyesho ya nane ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, Komba amesisitiza kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya watu au taasisi zinazojihusisha na utoaji wa mikopo kiholela isiyofuata sheria.

 “Nitumie fursa hii kutoa rai kwa wananchi kujenga utamaduni wa kutumia taasisi za kifedha zilizosajiliwa ili kupunguza machozi, manung’uniko na hasara ambazo wananchi wamekuwa wakizipata kwa kwenda kwenye taasisi zinazokopesha mikopo inayoumiza,” amesema Komba.

Akitolea mfano mji mdogo wa Katoro milani humo, DC Komba amesema kumekuwa na changamoto kubwa ya taasisi haramu zinazotoa mikopo kwa riba kubwa zisizo na usajili wowote, hali inayowafilisi wananchi na kuwaacha kwenye umasikini.

Katika ziara yake kwenye maonyesho hayo, Komba ametembelea banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambapo   ameipongeza  BoT kwa jitihada zao za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli za Benki hiyo . 

 “BoT wana kitengo maalum cha uchunguzi ambacho kazi yake ni kuhakikisha kuwa taasisi zote za mikopo zinazofanya kazi nchini zimesajiliwa na zinafuata sera za kifedha za Taifa letu,” alieleza.

Ameongeza kuwa, tayari kuna malalamiko kutoka kwa wananchi waliopoteza mali zao kutokana na mikopo kutoka taasisi feki huku akitolea mfano wa baadhi ya wajane waliopoteza nyumba zao baada ya kushindwa kulipa mikopo ya muda mfupi yenye riba kubwa, ambapo uchunguzi ulionyesha taasisi hizo hazikuwa zimesajiliwa.

“Kama serikali, tukigundua taasisi yoyote inayotoa huduma za kifedha bila usajili, tutawasiliana na BoT ili wachukue hatua za kisheria,hii ni kwa ajili ya kuwalinda wananchi wetu dhidi ya unyonyaji,” amesema Komba.

Aidha, ametahadharisha wananchi dhidi ya matapeli wa mitandaoni wanaotuma ujumbe mfupi (SMS) zenye ahadi za mikopo isiyokuwa na masharti magumu ili kuwavuta watu kwenye mitego ya kifedha.

 “Tusiwe watu wa kukimbilia fedha kwa haraka haraka kutoka taasisi zisizojulikana. Twende kwenye taasisi zinazotambulika ili, pale panapotokea changamoto, serikali iweze kusaidia,” ameongeza.

Katika ziara hiyo, DC Komba pia alikiri kufurahishwa na ushirikiano kati ya BoT na Bodi ya Bima ya Amana (DIB) katika kulinda wateja wanaoweka amana zao kwenye taasisi rasmi za kifedha, ambapo amesisitiza kuwa ni muhimu kwa wananchi kuwekeza fedha zao sehemu salama.