March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TARURA yaonyesha mafanikio na mikakati katika maonesho ya Teknolojia ya Madini Geita

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,GEITA

KATIKA maonesho ya nane ya kimataifa ya teknolojia ya madini yanayoendelea mkoani Geita, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wameonesha jitihada zao katika kuboresha miundombinu ya barabara nchini, hasa maeneo yanayohusiana na shughuli za uchimbaji madini. 

Akizungumza Septemba 24,2025 katika banda la TARURA kwenye maonyesho hayo,Meneja wa TARURA mkoa wa Geita, Mhandisi David Msechu, amesema ushiriki wao katika maonesho hayo ni kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yao na kazi wanazozitekeleza kwenye mtandao wa barabara za wilaya.

“Kwa sasa, TARURA inasimamia mtandao wa barabara zenye jumla ya kilomita 100,044 nchi nzima, ambapo katika mkoa wa Geita pekee kuna mtandao wa kilomita 7,264. Kati ya hizo, kilomita 564 zinahudumia maeneo ya madini, na asilimia 60 ya mtandao huo inapitika. “amesema Msechu

Msechu amesema kuwa barabara hizi ni muhimu kwa uchumi wa mkoa, hivyo wanajitahidi kuziendeleza kwa ujenzi, ukarabati na matengenezo endelevu.

“Katika mwaka wa fedha 2024/2025 na 2025/2026, TARURA imetenga Shilingi milioni 580 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kilomita 210 za barabara zinazoelekea kwenye maeneo ya madini ambapo amesema baadhi ya miradi hiyo imekamilika huku mingine ikiwa inaendelea, lengo kuu likiwa ni kuwezesha shughuli za kiuchumi na huduma za jamii kufanyika kwa ufanisi zaidi.

Pia amesema,TARURA inajivunia kuwa na maabara ya kisasa mkoani Geita ambayo inatumika kupima ubora wa kazi za barabara na miundombinu mingine ya umma. Msechu ameeleza kuwa maabara hiyo inahudumia miradi mbalimbali ya serikali ikiwemo ya umwagiliaji, TANESCO (power station ya Nakanyazi), miradi ya RUWASA, na pia miradi mikubwa ya TACTIC kama vile barabara ya lami ya kilomita 17 na ujenzi wa stendi ya kisasa.

Kwa mujibu wa Msechu,katika kuhakikisha matumizi ya teknolojia rafiki na ya gharama nafuu, TARURA Geita imeanza ujenzi wa madaraja kwa kutumia mawe, ambapo hadi sasa madaraja manne ya aina hiyo yamejengwa huku mengine yakiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Teknolojia hii inalenga kuongeza uimara wa miundombinu na kupunguza gharama za ujenzi.

Hata hivyo amesema, changamoto kubwa inayowakabili ni uharibifu wa barabara unaotokana na magari makubwa yanayopita katika barabara ambazo hazijajengwa kwa viwango vya kubeba uzito mkubwa zaidi ya tani 10. 

Msechu amesema wanaendelea na juhudi za kutenga fedha kwa ukarabati, lakini pia wanatoa wito kwa wamiliki wa migodi kushirikiana na TARURA kuboresha barabara hizo kwa pamoja.

Kwa upande wake, Mhandisi Faiza Mbande kutoka Makao Makuu ya TARURA amesema wako katika maonesho hayo kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi sahihi ya barabara. 

Amesema wanaelimisha wananchi kuhusu madhara ya kupitisha mizigo mizito, kulima pembezoni mwa barabara, pamoja na kulinda barabara dhidi ya uharibifu.

Faiza ameongeza kuwa wanatoa elimu juu ya masuala ya fidia kwa maeneo yanayohitaji kupisha miradi ya barabara. Amebainisha kuwa miradi mingi inatekelezwa kwa fedha za ndani na wakati mwingine haina kifungu cha fidia, hivyo ni muhimu wananchi kuelewa tofauti hiyo mapema.

Aidha, TARURA kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia inatarajia kutekeleza ujenzi wa barabara zenye jumla ya kilomita 59 katika Wilaya ya Mbongwe. Tayari usanifu wa barabara tatu umekamilika, ambazo ni Nyasumbwe-Mkweni, Nyomola na Kiseka-Isega, na kwa sasa wako kwenye hatua ya kumpata mkandarasi.