March 18, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

77 mbaroni tuhuma za kuhujumu miundombinu ya reli

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza

Jumla ya  watuhumiwa 77,wamekatwa  kwa tuhuma  za makosa mbalimbali ya jinai ikiwemo kuhujumu miundombinu ya reli,wizi wa mali za Shirika la Reli Tanzania (TRC),kupatikana na mali idhaniwayo ya wizi pamoja na dawa za kulevya(bangi).

Ni katika doria,misako na oparesheni zilizofanyika   Januari hadi Machi,2026 na  Jeshi la Polisi Kikosi cha Reli(T), katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Dodoma,Mwanza na Tabora.

Akizungumza Machi 18,2026 na waandishi wa habari mkoani Mwanza,Kamamda wa Polisi Kikosi cha Reli Tanzania,ACP.Matrida Kulyeto, amesema, Januari 12,2026 wilayani Bahi mkoani Dodoma,jeshi hilo liliwakamata  Martine Yohana na Malunde Luhende  kwa tuhuma za kubomoa nguzo 44, zinazoshikilia fensi ya SGR.

Ambapo waliiba nondo zilizokuwa ndani ya nguzo hizo na kwenda kuziuza kama chuma chakavu, watuhumiwa hao wamefikishwa  mahakamani kwa kosa la uhujumu uchumi.

ACP.Kulyeto,amesema Januari 31,2026, majira ya saa 10 jioni katika kiwanda cha Sayona Limited eneo la Nyahmg’omango, wilayani Misungwi mkoani Mwanza,walifanikiwa kuwakamata  watuhumiwa wawili wakiwa na gari lenye namba za usajili T.746 DFP,ikiwa na tela lenye namba T.869 CJL aina ya HOWO,likiwa limebeba vyumba chakavu.

Baada ya upekuzi kufanyika ulibaini kuwa limebeba vipande vya mabomba  ya chuma 68 ya kujengea madaraja ya reli,jeki 10 za  kujengea  madaraja ya reli,’lock’ za mabomba ,majongoo mawili ya kubania reli,vipande vya nondo saba,kipande cha chuma cha reli moja  na nati mbili za kufungia reli ambavyo ni mali ya shirika la reli vilivyoibwa mkoani Tabora.

Katika tukio jingine jeshi hilo liliwakamata Sali Mihangwa,Leonard Samson,Mbarouk Kaputula wote wakazi wa  Mkoa wa Tabora  pamoja na wenzao wanne kwa tuhuma za kuhujumu miundombinu ya Shirika la Reli Tanzania (TRC).

“Watuhumiwa hawa tuliwakamata Februari 10,2026 katika Kijiji cha Imalampaka wilayani Uyui mkoani Tabora,wakiwa na vyuma 15(fish plates) vya kuunganisha reli,vipande 963 vya ‘fish plates’ vilivyo katwa,vipande vya reli 13,’sole plates’ moja na shoka 303, zilizotengenezwa kwa kutumia vyuma vya reli katika viwanda vidogo vya kufuata vyuma,”amesema ACP.Kulyeto.

Pia amesema,tukio jingine ni Februari 11,2026 majira ya saa 11 na dakika tano jioni,huko katika stesheni ya SGR Igandu Wilaya ya Chawino mkoani Dodoma,walimkamata Masanja Kowo mkazi wa Ikule wilayani Mlimba mkoani Morogoro akiwa na dawa za kulevya aina ya bhangi gramu 12.5,alizokuwa anataka kusafiri nazo kwenye treni.

Mnamo Machi 16,2026 majira ya saa nne na dakika tano usiku huko kijiji cha Igumila Kata ya Ziba Wilaya ya Igunga mkoani Tabora  walimkamata Christina  Ngasa mkazi wa kijiji hicho akiwa na vipande 29 vya reli vilivyokatwa na mashine ya kysaga mawe(karasha 1),iliyotengeneswa kwa kutumia vyuma vya reli.

Sambamba na ukamataji huo,katika misako na oparesheni zinazoendelea kufanyika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mwanza,vimekamatwa  vifaa mbalimbali vya mradi wa reli ya SGR kipande cha tano,kinachoanzia Mwanza hadi Isaka.

“Vifaa hivyo ni madumu 105 yenye mafuta aina ya dizeli ujazo wa lita 20 kila Moja sawa na lita 2,092 yanayotumiwa kuendesha mutambo inayotumika katika ujenzi huo.Vitu vingine ni nondo 461 zenye ukubwa wa 10 mm,12 mm na 16 mm,vipande vya nondo 714,’binding wore rola’14,sub mita 5, marine board 4,betri ya jenereta  1 na mabomba ya chuma 51,”amesema ACP.Kulyeto.

Hata hivyo ACP.Kulyeto,amesema kwa kesi ambazo zilikuwa zinaendelea mahakamani mshtakiwa Julia’s Ishengoma, mfanyabiashara na mkazi wa Malampaka wilayani Maswali mkoani Simiyu alitiwa hatiani na kudhulumiwa kifungi cha miaka mitano hela na mahakama ya Wilaya ya Nyamagana Februari 26,2026 katika kesi ya jinai namba 7872 ya mwaka 2025 kwa kisa la kuhujumu miundombinu ya reli.

Kadhalika alitoa onyo kwa wachache wenye tabia na wanaoendekeza tabia ya kutofanya kazi halali za kujipatia kipato na kujiingiza kwenye uhalifu wa kuhujumu miundombinu ya shirika la reli kwani hawatasalimika na mkono wa sheria lazima uwafikie.

“Wanaojihusisha na biashara ya chuma chakavu wajiepushe na wizi au ununuzi wa mali za shirika la reli kwani kwa kufanya hivyo wanashiriki katika kuhujumu miundombinu hiyo,”amesema.