October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

64 mbaroni kwa tuhuma za kuhusika na biashara ya Q-net

Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online,Tanga

VIJANA wapatao 64 kutoka mikoa mbalimbali nchini wamekamatwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga kwa tuhuma za kujihusisha na uhalifu wa biashara isiyo halali ya kimtandao inayojulikana kama Q-net.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi, Dkt. Batilda Burian amesema vijana hao wamekuwa wakiwapigia simu wazazi na kuwataka kutoa fedha ili vijana wao waweze kupata ajira kupitia bidhaa zao wanazouza.

Dkt. Buriani amefafanua kuwa vijana hao wakiwemo wavulana 29 na wasichana 35, viongozi wao wapo jijini Dar-es-salaam wakati mikoani wakiwatuma wao kufanya kazi hiyo.

“Tumeona vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa, kuanzia miaka 19 hadi 24 na wengine wamefika hadi vyuo vikuu lakini hakuna wanachofanya, kazi ni hiyo ya utapeli,”amesema Dkt. Buriani.

Pia ametoa rai kwa wazazi kuwa makini endapo kama watapigiwa simu na watu wasiowajua wakidai kutoa nafasi za ajira hasa za kimtandao.

“Huu utaratibu wa wazazi mnapigiwa simu kuna nafasi za kazi na ninyi mnawaruhusu wanakwenda, huu ni utapeli mtupu tuweni makini hasa na mitandao,”.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa vijana wote waliokamatwa watasaidiwa kupatiwa mafunzo katika vyuo vya veta ili kuweza kupata elimu ya ujasiriamali itakayowasaidia kupata ujuzi katika maeneo yao.

“Tanga ni Mkoa salama na hakuna nafasi ya kufanya biashara ambazo hazitambuliki, lakini pia vijana hawa watarudishwa katika maeneo yao chini ya uangalizi maalumu,” amesisitiza.