January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

6 Mbaroni kwa kuchoma moto nyaraka

Na Daud Magesa Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

WATU 6 wamekamatwa wilayani Ukerewe wakidaiwa kuchoma moto nyaraka mbalimbali za ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata ya Kagunguli.

Akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro alithibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao.

Amesema watu sita bila kuwataja majina, wanashikiliwa na jeshi la polisi wilayani Ukerewe kwa tuhuma za kuvunja mlango wa jengo la ofisi ya Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kagunguli na kuchoma nyaraka mbalimbali za ofisi hiyo.

“Watuhumiwa hao walikamatwa baada ya kuchoma karatasi (nyaraka) mbalimbali kwenye ofisi hiyo ya Mtendaji wa Kata wakihisi kulikuwa na karatasi za ziada za kupigia kura,kabla ya kufanya tukio hilo walivunja mlango wa jengo hilo lenye ofisi sita,”amesema Muliro.

Amesema  jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo utakapokamilika litawafikisha mahakamani kwa mujibu wa sheria ili kujibu tuhuma zinazowakabili.

Wakati huohuo Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewapongeza wadau wa uchaguzi mkoani humu kwa kufanya uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu.   

Muliro alitoa kauli hiyo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na uchaguzi mkuu uliofnyika Oktoba 28, mwaka huu.

Amesema katika Mkoa wa Mwanza,jeshi l polisi liliimarisha usalama kwa kiwango cha juu na kuufanya uchaguzi mkuu wa mwaka huu,kufanyika kwa haki, uhuru,amani na utulivu bila bughudha.

“Jeshi la polisi linawapongeza wadau wa uchaguzi ambo walitoa taarifa mbalimbali za watu waliokuwa wakipanga njama za kufanya vurugu na fujo ambo walikamatwa na kuhojiwa baadaye kuachiwa kwa dhamana na kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani,hakuna matukio makubwa ya ajabu ya kuathiri mchakato wa uchaguzi mkuu,”amesema Muliro.

Amesema jeshi hilo linafuatilia kwa karibu mchakato wote wa uchaguzi mkuu 2020, kabla, wakati na baada ya kupiga kura katika wilaya na majimbo yote na zipo taarifa za vikundi ama watu kupanga kufanya vurugu.

Muliro amesema wanaendelea kufuatilia mienendo ya taarifa za watu wanaodaiwa bado wana mipango ya kutaka kufanya fujo au vitendo vya kihalifu.

Alieleza kuwa jeshi hilo halitamvumilia mtu yeyote ama kikundi chochote kitakachobainika kuandaa mipango ya kufanya vitendo vyovyte vinavyokinzana na sheria za nchi.

“Polisi hawataruhusu kundi la watu kula njama za kufanya fujo baada ya matokeo yote ya uchaguzi kutangazwa, watakaothubutu watajiingiza kwenye mgogoro na msuguano na jeshi la polisi, hatutakubali watu kuingia barabarani na hatutamvumilia yeyote na atakayethubutu kupanga njama hizo za vurugu,”amesema Muliro.

Amewataka wananchi mkoani Mwanza kuwa watulivu na kufanya shughuli zao za uzalishaji na kiuchumi kwa uhuru kwa sababu jeshi la polisi liko mitaani na limeimrisha usalama kwa kiwango cha juu kuhakikisha amani na utulivu unakuwepo muda wote.