December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani akitoa maelekezo kwa Mhandisi wa Tanesco, Ramadhani Kidunda wakiwa wanakagua njia ya kusafirisha umeme kutoka kituo cha kupozea umeme Mpomvu Geita kwenda GGML. (Picha na Mutta Robert).

Waziri Kalemani aiagiza GGML kujenga kituo cha kupozea umeme ndani ya mwezi mmoja

Na Mutta Robert,TimesMajira Online,Geita

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani ameiagiza Kampuni ya Uchimbaji wa Dhahabu ya Geita (GGML) kuhakikisha inajenga kituo cha kupozea umeme na kuingiza katika mgodi huo katika shughuli zake ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa.

Waziri Kalemani ametoa agizo hilo akiwa kwenye ziara katika mgodi huo kukagua maendeleo ya ujenzi wa njia ya kupeleka umeme unaosafirishwa kutoka kituo cha Tanesco cha kupozea umeme cha Mpomvu, Geita mjini kuelekea GGML.

Mgodi huo unahitaji umeme wa kilovoti 33 kutoka Tanesco ili kuendeshea kitambo yake inayotumika katika kazi za kuchimba na kusaga mawe ya dhahabu na shughuli nyingine za mgodini huo.

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani akitoa maelekezo kwa GGML kwenye kikao cha ndani mgodini hapo.Mwenye shati ya kijani ni Naibu wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Costantine Kanyasu na Mbunge wa Geita Mjini. (Picha na Mutta Robert).

Hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Dkt.Tito Mwinuka amesema kuwa, shirika hilo linatarajia kuwa linapata zaidi ya sh.Bilioni 6 kila mwezi kutoka GGML kutokana na mauzo ya umeme katika mgodi huo baada ya ujenzi wa kituo cha kupozea umeme kinachojengwa Geita kukamilika.

Mtaalam wa mgodi huo,Mhandisi Mwandamizi wa Uhandisi, Maftah Seif akitoa ufafanuzi wa kitaalamu kwa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani kuhusu ujenzi wa kituo cha kupozea umeme cha GGMLamesema kuwa, mgodi huo unatumia zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 3.2 kila mwezi kununua mafuta ya kufua umeme wa kuendeshea shughuli zake.

Amesema kuwa, endapo mgodi huo utapata umeme huo wa Tanesco wataokoa zaidi ya dola za Kimarekani Milioni 1 kwa kila mwezi ambazo zilikuwa zinatumika kununua mafuta ili kufua umeme kwa shughuli zake.

Mhandisi Maftah amefafanua kuwa, mgodi huo uko tayari kujenga kituo cha kupokelea umeme na kupoza (substation) mgodini hapo na gharama za mradi huo zinakadiliwa kufikia dola za Kimarekani milioni 14.

Mhandishi Maftah Seif akaomba Waziri wa madini akubaliane na ratiba ya mgodi huo wa kutumia miezi 18 kukamilisha mradi huo kwani kwa sasa wako katika hatu za upembuzi na bado hatua za manunuzi na ujenzi.

Ameongeza kuwa,Transfoma pekee ya kupokelea umeme huo kuingia mgodini hapo ili kuinunua inahitajika takribani miezi minane hadi kumi hadi kufikishwa mgodini hapo kwa ajili ya kusimikwa.

Waziri Kalemani alikataa ombi hilo na kuagiza mgodi huo kuhakikisha hadi kufikia mwezi Julai mwaka huu umeme uwe umeingizwa katika mgodi na kuanza kutumika katika kazi uchimbaji.

Dkt.Kalemani amesema kuwa, Serikali inategemea kukusanya mapato ya kutosha kutoka mgodini hapo baada kuuza umeme, lakini gharama za uendeshaji za mgodi zitapungua hivyo kodi za serikali zitaongezeka.

Tanesco inajenga na kusafirisha umeme wa kilovoti 220 kutoka kituo kikuu cha Bulyanhulu hadi Geita ambao kilovoti 33 zinapelekwa kwenye mgodi wa GGML.

Mhandisi wa Tanesco anayesimamia eneo la mradi, Ramadhan Kidunda amesema ujenzi wa njia ya kufikisha umeme GGML kutoka kituo cha Mpomvu cha kupozea umeme ni kilomita 6 na ujenzi umekamilika kwa kilomita 5 bado kilomita 1 ambayo inatarajia kukamilika mwezi Julai.

Waziri Kalemani amekagua njia hiyo ya kupeleka umeme GGML na kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa ujenzi huo na kuagiza ujenzi ukamilike kwa wakati.