November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

500 kufanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho Mbarali

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbarali

WAGONJWA takribani 500 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho wilayani Mbarali mkoani Mbeya kutoka kwa madaktari bingwa wa macho ambao wameweka kambi ya wiki moja katika Wilaya hiyo .

Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa kambi ya mtoto wa jicho Mkuu wa Wilaya ya Mbarali,Kanali Dennis Mwila amesema kuwa kambi hiyo itadumu kwa muda wa siku Saba wilayani humo.

Kambi hiyo ilianza Agosti 14 mwaka huu na inatarajiwa kumalizika Agosti 20 mwaka huu, ambapo wakazi wa Wilaya hiyo wanaendelea kupata nafasi ya kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu ya upasuaji wa mtoto wa jicho.

Amesema kuwa tatizo hilo ni kubwa kwa Wilaya ya Mbarali ambapo mwaka 2022 waligundua watu wenye mtoto wa jicho 1,750 kati ya hao walikuja kwa awamu tatu kuweza kutibiwa na kwamba awamu ya tatu walitibiwa wagonjwa 800 sawa na asilimia 65 ya wagonjwa wote waliopo katika Wilaya hiyo.

“Gharama ya kumtibu mtu mmoja ni dola 98 ambayo ni sawa na shilingi 220,000 kwa hiyo hii kambi iliyoanza jana imeweza kutibu watu 70 na inategemea kuisha Agosti 20 ambapo watu 500 watakuwa wametibiwa na zitatumika zaidi ya milioni 110,”.

Baadhi ya agonjwa waliofanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kambi hiyo, Kanali Mwila amesema kulingana na taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) asilimia moja ya watu wanapata matatizo ya macho.

Aidha, Kanali Mwila amelipongeza Shirika la Kimataifa la Helen Killer kwa kuanza kampeni ya kutokomeza magonjwa ya macho Juni 2022 ambapo wametoa vifaa vyenye thamani ya milioni 140 kwa Mkoa wa Mbeya pamoja na mafunzo kwa watumishi wa afya ngazi ya jamii wapatao 570.

Amesema, kwa mwaka jana (2022) watu 29,000 walionwa katika Mkoa Mbeya katika yao wagonjwa 3,406 walikuwa na tatizo la mtoto wa jicho na magonjwa mengine.

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Kanali Dennis Mwila

Naye, Meneja Mpango wa Taifa wa Macho kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Bernadetha Shilio amesema kuwa mbinu inayotumika kuwapata wagonjwa ni kupitia wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambao wanaambatana na wataalamu wa afya nyumba kwa nyumba na kuwabaini wagonjwa.

Dkt. Shilio amesena kuwa huduma za upasuaji katika kambi hiyo ya siku saba katika Hospitali ya Wilaya ya Mbarali zinatolewa bila malipo chini ya ufadhili wa Shilika la Kimataifa la Helen Killer.

Amesema kuwa wao kama Wizara ya Afya wamekuwa wakifanya kazi kwa kushirikiana na wadau kuhakikisha huduma za macho zinawafikia wananchi mahali walipo na wameweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa Wilaya ya Mbarali ambayo ni mfano wa tofauti kwani wanafuata kwenye makazi yao na kuwatambua inapogundulika wana mtoto wa jicho wanapelekwa hospitali kwa Wilaya kwa ajili ya upasuaji.

Meneja mradi shirika la Helen Keller International ,Athuman Tawakal amesema kuwa mradi huo ulianza Juni 2022 kwa kukabidhi vifaa tiba kwa hospitali Rufaa Kanda ya Mbeya pamoja na hospitali ya Wilaya ya Mbarali ambapo vifaa hivyo vinatumika katika kutoa huduma na baadaye waliendelea kutoa mafunzo kwa wahudumu ngazi ya jamii ambao wanasaidia kupita kaya kwa kaya kutambua wagonjwa wa mtoto wa jicho katika maeneo mbalimbali .

Aidha Tawakal amesema baada ya hapo walianza kuweka kambi ya matibabu ambayo ya awamu ya kwanza ilikuwa Septemba mwaka 2022 na malengo makuu ya mradi ilikuwa kufikia wagonjwa 900 kwa Wilaya ya Mbarali na walivyoanza kambi ya kwanza walianza kwa mafanikio makubwa.

‘’Tumeanza kambi yetu ya kwanza kwa kuwafikia wagonjwa 291 na mpaka kufikia leo tumeshafanya kambi tatu za matibabu na jumla ya wagonjwa 882 wameshafanyiwa matibabu na wameweza kuona tena katika wilaya hii ya Mbarali ,tuliona ipo haja ya kuongeza kambi ya nne ambapo tunalenga kufikia wagonjwa 500,’’amesema.

Kwa upande wake Kaimu Mratibu wa macho Ofisi ya RaisTAMISEMI, Ernest Paul amesema Serikali itahakikisha inawezesha upatikanaji wa huduma za macho karibu na wananchi hususani ngazi ya msingi.

Mkazi wa Mbarali aliyefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho , Mwigulu Mjengwa amesema kuwa amekuwa na tatizo hilo la macho kwa muda wa miaka mitatu hali iliyompelekea kutokuona kabisa mpaka kushindwa kuwatambua mpaka watoto wake kutokana na tatizo hilo.