December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

4R za Rais Samia zaifikia sekta ya habari, utangazaji

Na Penina Malundo, Timesmajira Online

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Kabudi Palamagamba, amesema sekta ya habari na utangazaji ipo tayari kuishi katika dhima ya Rais Samia Suluhu Hassan ya 4R,kwa lengo la kufanya maridhiano, uvumilivu, kuleta mageuzi na ujenzi mpya ili Tanzania izidi kusonga mbele na watanzania wapate yale wanayoyatarajia katika nchi yao.

Ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wadau wa habari na utangazaji.

Prof. Kabudi alisema tangu 4R hizo kutangazwa na Rais Samia kumekuwa na ushirikiano mkubwa kati ya Sekta ya habari na wadau wa habari katika masuala yanayohusu kuboresha sera ,sheria na kanuni.

Prof.Kabudi alisema kuongezeka kwa uhuru wa habari na ukuaji wa sekta ya habari nchini ni moja ya mafanikio ya serikali ya awamu ya sita.’

‘Kuwepo uhuru wa habari nchini ambayo inalindwa na ibara ya 18 ya Katiba ya nchi inayoeleza kila Raia anahaki ya kupata taarifa wakati wowote.

”Kutokana na usimamizi mzuri wa sekta ya habari nchini,imeweza kupiga hatua kubwa katika kuimarisha uhuru wa habari ambapo kwa Mujibu wa Ripoti ya uhuru wa vyombo vya habari dunia ya mwaka 2024, Tanzania imekuwa ya 57 kwa mwaka huu kutoka 145 kwa mwaka 2023,”alisema

Alisema ataendeleza juhudi hizo na kupanda nafasi za juu kabisa ili nchi ya Tanzania iweze kupata sifa kubwa zaidi.”Kutokana na takwimu hizi ambazo zinaonesha tunazidi kupanda,natamani Tanzania iwe namba moja ya nchi kinara sio bara la Afrika bali duniani katika uhuru wa vyombo vya habari,”alisema.

Alisema taifa lolote linalijitambua kama ilivyo Tanzania lazima iipe sekta ya habari nafasi maalum.

Kwa Upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema vyombo vya habari zaidi ya 1200 vimesajiliwa na kuajiri makundi mbalimbali ya watu wakiwemo watangazaji na mafundi mitambo.

Msigwa alisema serikali inaendelea kuboresha sekta hiyo ili kuleta mabadiliko chanya kwa kufanya marekebisho ya baadhi ya sheria za habari

Alisema sekta ya habari imekuwa ikichangia mapato ya serikali kupitia kodi na matangazo na huduma mbalimbali