Na Mwandishi wetu, timesmajira
JUMLA ya wanagenzi 362 wamenufaika na mafunzo ya Uanagenzi Pacha kwenye fani ya Ufundi wa Zana na Mitambo ya Kilimo kupitia mradi uliotekelezwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Taasisi ya Kijerumani ya “West German Skills Craft (WHKT)” katika vyuo vitano (5) vya VETA vya Manyara, Kihonda, Dakawa, Arusha na Mpanda.
Hayo yamebainishwa,jana tarehe 19 Machi 2024 na Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi wa VETA, Abdallah Ngodu, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa VETA kwenye hafla ya kuhitimisha mradi huo iliyofanyika kwenye Chuo cha VETA cha Mkoa wa Manyara, kilichopo mjini Babati.
Mafunzo ya Uanagenzi hutolewa kwa utaratibu wa kupokezana wanafunzi (wanagenzi) kati ya vyuo na mahala pa kazi, ambapo katika mradi huo wanagenzi walikuwa wakihudhuria mafunzo kwenye karakana za vyuo kwa kipindi maalum, kisha kwenda kwenye mafunzo ya vitendo katika viwanda na mashamba ya kilimo.
Amesema Mafunzo hayo hutolewa kwa kipindi cha miaka mitatu ambapo kwa kila mwaka wanagenzi wanatumia wiki 20 kwa mafunzo chuoni na wiki 32 kwa mafunzo ya sehemu ya kazi.
Ngodu ameyataja manufaa mengine yaliyopatikana kupitia mradi huo kuwa ni pamoja na walimu wa VETA kupatiwa mafunzo katika ngazi ya kitaifa na kimataifa ili kuwawezesha kutoa mafunzo bora yanayokidhi mahitaji ya makampuni na viwanda, pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kilimo kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia.
Ameongeza kuwa wananchi wa mikoa vilivyopo vyuo vilivyotekeleza mradi wamepata fursa ya kujifunza juu ya matumizi na utunzaji wa zana na mitambo ya kilimo pamoja na mbinu za kuzuia upotevu wa mazao baada ya mavuno (Prevention of Post-harvest Losses).
Ameishukuru Serikali ya Ujerumani kwa kuwezesha utekelezaji wa mradi huo na kusisitiza kuwa VETA itaendelea kutumia mfumo huo kama mbinu mojawapo ya kutoa mafunzo katika vyuo vyake.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Taasisi ya WHKT ya Ujerumani, Bastian Hermans amesema Ujerumani inajivunia kuanzisha mfumo huo hapa nchini na kwamba WHKT imefurahia mafanikio yaliyotokana na utekelezaji wa mradi huo.
Muasisi wa Mradi huo kwa upande wa Ujerumani, Herman Roeder ametoa wito kwa VETA kutumia vyema uzoefu walioupata katika utekelezaji wa mradi huo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018 ili kuboresha zaidi utoaji mafunzo na kuzalisha vijana wenye ujuzi katika kutumia zana na mitambo ya kilimo.
Kwa upande wao wadau wa kilimo walionufaika na mradi huo wameishauri VETA kuendeleza na kupanua wigo wa utoaji wa mafunzo kwa mfumo huo ili kuzalisha nguvukazi kwa ajili ya kuhudumia sekta ya kilimo ambayo itasaidia kukuza na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao na kuchangia uchumi wa nchi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Kilimo Tanzania na Mkurugenzi wa kampuni ya Kavel Coffee Plantation Ltd ya mkoani Manyara, Jitu Soni, amekiri kuwa mafunzo ya uanagenzi kwenye ufundi wa zana za kilimo yamewezesha makampuni ya kilimo kupata vijana wenye ujuzi wa kutumia na kuhudumia zana na mitambo ya kilimo na hivyo kuchangia kuongeza tija katika Sekta ya Kilimo.
“Kupitia mfumo huu tumepata vijana wazuri sana wenye utaalamu wa kuhudumia zana za kilimo na kufanya ukarabati wa vifaa vya kilimo na hivyo kutupa uhakika wa kuendesha shughuli zetu,” amesema.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Oljoro Plantations Ltd ya Jijini Arusha, Ray Travas, ametoa wito kwa Serikali kuongeza wigo wa utoaji mafunzo kupitia mfumo huo ili kuihakikishia Sekta ya Kilimo upatikanaji wa nguvu kazi yenye utaalamu wa kutumia na kutunza zana na mitambo ya kilimo na kuongeza tija kwenye kilimo.
Mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mjumbe wa Bodi ya VETA, Mhandisi Ezekiel Kunyaranyara, amesema Wizara itaendelea kuweka msisitizo na kuwezesha utoaji mafunzo kwenye Sekta ya Kilimo ili kuwezesha upatikanaji wa wataalamu mahiri watakaohudumia sekta hiyo kwa ufanisi na kuongeza tija.
Mhandisi Kunyaranyara ametoa wito kwa wahitimu wa VETA kujiunga kwenye vikundi na kuanzisha shughuli mbalimbali kulingana na fani walizosoma ili kuwawezesha kujipatia mikopo inayotolewa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya kuendeleza shughuli za uzalishaji.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini