Na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU Chamwino
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, Mjane wa Baba wa Taifa Mama Maria Nyerere, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili   Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu   Benjamin William Mkapa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne   Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete leo tarehe 30 Mei, 2020 wameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi Kuu za Ikulu, Mkoani Dodoma.
Majengo 6 ya Ofisi za Ikulu yaliyounganishwa yanajengwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika eneo la Vikonje Jijini Dodoma kwa usanifu na muonekano sawa na majengo ya Ofisi za Ikulu Jijini Dar es Salaam, na yanatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 5 ijayo.
Ujenzi wa majengo ya ofisi hizo ni sehemu ya ujenzi mkubwa wa Ikulu Mkoani Dodoma, na tayari majengo mengine mbalimbali ikiwemo nyumba ya makazi ya Rais, Ofisi mbalimbali na uwigo wa ukuta (Fence) wenye urefu wa kilometa 27 yamekamilika na yanatumika.
Katika hotuba yake, Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa kazi nzuri ya ujenzi wa Ofisi hizo pamoja na majukumu mengine ya ujenzi na uzalishaji mali wanayoyatekeleza, na ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada hizo.
Rais Magufuli ameipongeza Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) ambayo ni mkandarasi mshauri wa mradi huo na amemuagiza Waziri wa Fedha Dkt. Philip Mpango kutoa shilingi Bilioni 2 zitakazoungana na shilingi Bilioni 1 zilizotolewa awali ili JKT kupitia shirika lake la SUMA-JKT wakamilishe ujenzi katika kipindi cha miezi 5 walioahidi.
Rais Magufuli amewashukuru Mama Maria Nyerere na Marais Wastaafu kwa kuhudhuria sherehe za uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi hizo na kutembelea maeneo ya Ikulu ya Chamwino ambapo wamejionea kazi iliyofanyika kujenga miundombinu na majengo ikiwemo makazi ya Rais.
Rais Magufuli ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano iliamua kuchukua hatua madhubuti za kutekeleza azimio la Serikali kuhamia Dodoma kama alivyoahidi mwezi Julai 2016 ambapo tayari Wizara zote, watumishi, viongozi wakuu akiwemo yeye mwenyewe wamehamia Dodoma, na kwamba kutokana na mafanikio hayo ameona ni vema jengo kuu la Ofisi za Ikulu lijengwe kwa mfano uleule wa Ikulu ya Dar es Salaam ili kutunza historia.
Aidha, Rais Magufuli amesema Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere alipotangaza uamuzi wa kuhamia Dodoma na kujenga Ikulu ya Chamwino, alichukua eneo la ekari 61 ambalo lilikuwa ni kubwa zaidi ya ekari 41 za Ikulu ya Dar es Salaam, lakini baada ya yeye kuamua kutekeleza uamuzi huo ameongeza eneo hadi kufikia ekari 8,473, amejenga kilometa 27 za ukuta wa kuzunguka eneo lote, amejenga barabara za lami na ameweka wanyama mbalimbali wakiwemo pundamilia, twiga, swala, sungura pori, kudu, batamaji na aina mbalimbali za ndege.
Rais Magufuli amebainisha kuwa ukubwa wa Ikulu ya Chamwino (ekari 8,473) ni zaidi ya mara 15 ya ukubwa Hifadhi ya Taifa ya Saanane yenye ukubwa ekari 533 na kwamba kutokana na uwepo wa wanyamapori na mandhari ya kuvutia, Ikulu ya Chamwino inaweza kutumika kama kivutio cha utalii
Katika salamu zao, Marais wastaafu na familia ya Baba wa Taifa (salamu zimewasilishwa na Ndg. Makongoro Nyerere) wamempongeza na kumshukuru Rais Magufuli kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuhamisha Serikali yote kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma pamoja na kujenga majengo na miundombinu mbalimbali ya Ikulu, Chamwino ikiwemo Ofisi Kuu ya Ikulu.
Sherehe hizo, zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Ibrahim Hamis Juma, Mawaziri Wakuu Wastaafu ( John Samwel Malecela na Mizengo Kayanza Peter Pinda), Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi, Makatibu Wakuu, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (Bara) Ndg. Philip Mangula na Katibu Mkuu wa CCM Ndg. Bashiru Ally Kakurwa.
Mapema, Mama Maria Nyerere (kwa niaba ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere), Rais Mstaafu Mwinyi, Rais Mstaafu Mkapa na Rais Mstaafu Kikwete walikabidhiwa ndege aina ya Tausi 25 na kilo 100 za chakula cha Tausi kwa kila mmoja kwa ajili ya kwenda kuwafuga katika bustani zao. Viongozi hao waandamizi wamemshukuru Rais Magufuli kwa kuwapa ndege hao.
Ndege aina ya Tausi ambao waliletwa nchini na Baba wa Taifa hayati Mwl. Nyerere wameongezeka kwa idadi kubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kutoka 403 hadi 2,260 na hivi sasa wanawekwa katika Ikulu ndogo za hapa nchini.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote