January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya

Na Agnes Alcardo,Timesmajiraonline,Dar

VIJANA 15 wa kitanzania wamekwea ‘Pipa’ kwenda katika Jiji la Turin nchini Italia kwa ajili ya mafunzo ya mpira wa miguu yanayoendeshwa na Shule ya Michezo ya Klabu ya Juventus iliyopo nchini Tanzania.

Akizungumza na Gazeti la Majira kwa njia ya simu mapema Desemba 18, 2024 kijana wa kitanzania Aaron Patrick (16),amesema amefurahishwa na hatua iliyofanywa na ‘Juventus Academy’nchini Tanzania ya kutambua vipaji vyao katika uchezaji wa mpira wa miguu na kuwapeleka Italia kwa ajili ya mafunzo zaidi.

Amesema, katika kipindi cha siku 14 akiwa nchini Italia, atautumia muda huo wa mafunzo vizuri, ili kuhakikisha anafikia malengo yake ya kuja kuwa mchezaji mkubwa wa mpira wa miguu na kuchezea katika moja ya timu kubwa nchini Tanzania na ‘team’ za nchi za nje ikiwemo Liverpool.

“Napenda sana mpira wa miguu na ninauweza hasa na ndoto yangu ni kuona siku moja nakuwa mchezaji mkubwa wa mpira wa miguu na kuchezea timu yangu ya Taifa na naahidi endapo nitafanikiwa basi nitaisaidia timu yangu kufika kucheza mpaka kombe la dunia na endapo nitatimiza ndoto yangu basi nitafanya makubwa zaidi kwa nchi yangu katika upande wa michezo”, amesema Aaron.

Aaron ambaye pia ni mwanafunzi katika Chuo cha Biashara (CBE) Kampasi ya Dar es Salaam, ambaye amekiri kurithi kipaji cha mpira wa miguu kutoka kwa Baba yake, Patrick Mwalunenge, amewasihi vijana wengine kuishi katika ndoto zao ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea, ikiwa pamoja na kusoma kwa bidii, kukuza vipaji vyao na kuachana na mambo ya anasa kama uvutaji wa sigara na matumizi ya vilevi.

“Mimi nimerithi mpira kutoka kwa baba yangu kwani yeye pia alikuwa mchezaji wa mpira hapo zamani kabla ajaingia katika masuala ya siasa, hivyo wito wangu kwa vijana wenzangu ni kuwa na heshima, nidhamu na kutambua wanafanya nini, vijana wengi wa Tanzania wanasema mpira ni ‘connection’ wakati siyo kweli, ukifanya vizuri utaonekana tu muhimu ni kujitambua na kuachana na mambo ya anasa kama uvutaji wa sigara na matumizi ya vilevi kwani hivyo vyote haviendani na mpira”.

Mimi mpaka nimeonekana na kuwa miongoni mwa waliochaguliwa kuja huku nchini Italia kwa ajili ya mafunzo ya mpira wa miguu ni pamoja na nidhamu yangu niliyonayo kwa kila mmoja lakini pia mbali na yote hayo wasome kwa bidii kwani elimu ndiyo kila kitu kwa dunia ya sasa”, ameongeza Aaron.

Aidha, Baba mzazi wa Aaron ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge, akizungumzia kipaji cha Aaron amesema, walikigundua kipaji hicho tangu Aaron akiwa mtoto.

Amesema, Aaron aligundulika kuwa na kipaji cha kucheza mpira wa miguu tangu alipokuwa mtoto mdogo, ambapo wao kama wazazi walipogundua waliamua kukiendeleza hadi kufika hapo, huku wakielezea matumaini yao ni kumuona kijana wao anakuja kuwa mchezaji mkubwa wa mpira wa miguu ndani na nje ya nchi.

“Mimi kama mzazi ni wajibu wangu kumsomesha mtoto wangu kupata elimu lakini pia kama ana kipaji basi kukiendeleza na ndivyo nilivyofanya kwa huyu na ndivyo pia nitakavyofanya kwa vijana wangu wengine”.

Aaron tulimuona na kipaji cha mpira wa miguu tangu akiwa ni mdogo mwenye umri wa miaka 5, hivyo tulifurahi na tukaona kuna umuhimu wa kumuendeleza na tunashukuru Mungu anafanya vizuri na tunatumai kuona mazuri zaidi katika safari yake ya mpira.