Na Angela Mazula,TimesMajira Online, Dar es Salaam
WASHINDI 12 wa droo ya saba ya Kampeni Weka Akiba na Ushinde ‘NMB Bonge la Mpango’, inayoendeshwa na Benki ya NMB, wamepatikana leo, ambapo wawili walijinyakulia pikipiki za miguu mitatu aina ya Lifan Cargo.
Droo hiyo imefanyika kwenye Tawi la Mbezi Louis jijini Dar es Salaam, ambako idadi hiyo inafanya jumla ya wateja 82 kunufaika na NMB Bonge la Mpango, wakiwemo 70 waliojinyakulia pesa taslimu na washindi 14 waliotwaa zawadi ya pikipiki ya miguu mitatu.
Akizungumza kabla ya kufanyika kwa droo hiyo, Meneja Mwandamizi wa Bima wa Benki ya NMB, Catherine Joshua, amesema hadi sasa wametoa zawadi zenye thamani zaidi ya Sh. Mil. 109, tangu kuanzishwa kwa NMB Bonge la Mpango, kampeni itakayotoa zawadi za Sh. Mil. 550 hadi itakapofikia ukomo.
“NMB Bonge la Mpango ni kampeni inayo hamasisha utamaduni chanya wa uwekaji akiba, ambako washindi 10 kila wiki hujishindia pesa taslimu, pamoja na pikipiki ya Lifan Cargo, sambamba na gari dogo ya mizigo (maarufu Kama Kirikuu) katika droo za kila mwezi.
Catherine amesema, ipo zawadi kuu ambayo ni gari la kifahari aina ya Toyota Fortuner yenye thamani ya Sh. Mil. 169 na kuwataka wateja kuendelea kuweka akiba inayoanzia Sh. 100,000 katika akaunti zao na kwa wasio na akaunti, kufungua na kuweka akiba kuanzia kiasi hicho ili kujiwekea nafasi ya kushinda.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Elibariki Sengasenga, amewahakikishia wateja wa NMB kuwa Bonge la Mpango ni kampeni inayoendeshwa kwa mujibu wa sheria, ukizingatia taratibu zote na kuwataka kushiriki bila hofu, kwani inafanyika chini ya usimamizi wao.
“Niko hapa kwa ajili ya kusimamia droo hii, ambako ni jukumu letu kama Bodi yenye dhamana na niwahakikishie washiriki kuwa kampeni hii inatoa washindi kwa kufuata taratibu zote, wito wetu kwao ni kuendelea kujiwekea akiba, ambacho ni kigezo kikuu cha kupata nafasi ya kushiriki,” amesema Sengasenga.
Katika droo hiyo, waliojinyakukia pesa taslimu ni: Imelda Christopher Laizer na Annastazia George Lukinga (500,000), Marietta Kashindye Ndanshau (129,391.60), Mary Tungucha (300,000), Sawiya Rashid Mtawala ( 407,200 ).
Washindi wengine wa pesa taslimu wa droo ya saba ni: Joyce Massawe Edesi (298,200), Linus William Rwinwa (298,200) Jonas John Dasare (202,300) ,Bernadetha Philipo William (304,200) na Letinga Matangi Lyama ( 104,933)
Katika droo hiyo, washindi wawili walioshinda pikipiki za Lifan Cargo walikuwa ni Emmanuel Enos Mwavipa mkazi wa Bariadi na Kijiwe Mishkaki.
NMB Bonge la Mpango ni kampeni ya miezi mitatu iliyozinduliwa mapema mwezi wa tatu (Machi) mwaka huu, ambako licha ya kuhamasisha utamaduni chanya wa kuweka akiba, inatumiwa pia na Benki hiyo kurejesha kwa jamii sehemu ya faida yake ya mwaka.
More Stories
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25