November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

12 mbaroni kwa kukutwa na simu zaidi ya 300 zinazodhaniwa za wizi

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza 

Watu 12 wanashikiliwa wakiwemo mafundi simu na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza  kwa kukutwa na simu 309 na vifaa vingine mbalimbali   vinavosadikiwa kuwa ni mali ya wizi.

Akizungumza  Agousti 12,2023  na waandishi wa habari mkoani Mwanza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza SACP.Wilbord Mutafungwa ameeleza kuwa wamekuwa wakipata taarifa kutoka kwa wakazi wa Mwanza hususani wa Wilaya ya Ilemela na Nyamagana kwamba katika mitaa ya Lumumba na Sahara wapo watu wanaojihusisha na vitendo vya kununua na kumiliki vifaa  vya wizi ambavyo ni simu za mkononi  pamoja na vifaa vingine kama kompyuta.

“Kufuatia taarifa hizo ambazo tumekuwa tukizipokea mara kwa mara tukaamua kufanya msako na  kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao wakiwa na simu hizo ambazo zinadhaniwa kuwa ni mali ya wizi,”ameeleza Mutafungwa.

Pia wamefanikiwa kuwakamata mafundi  wawili wa simu ambao wamekutwa na vifaa mbalimbali vya ufundi  pamoja na simu zinazodhaniwa kuwa ni mali ya wizi.

Ameeleza kuwa pamoja na kuwakamata watuhumiwa hao bado operesheni inaendelea  katika maeneo hayo  yaliotajwa pamoja na Wilaya nyingine kuhakikisha kwamba watu  wanaojihusisha na kupokea mali za wizi hususani simu na vifaa vingine wanakamatwa ili kupunguza wimbi la watu kutibiwa simu za mikononi.

Aidha ameeleza kuwa watuhumiwa hao pia  wamekatwa wakiwa na vifaa na simu mbalimbali ambazo zimetumika bila ya kuwa na nyaraka muhimu ambazo zinaonesha uingizwaji wa simu hizo.

“Jeshi la Polisi tumebaini kuwa watuhumiwa hao ni wapokeaji wa simu na vifaa vilivyo tumika na baadhi yao leseni zao za biashara zinaonesha kuwa wanatakiwa kuuza vifaa  vya simu  na siyo simu kama ambavyo wanafanya kwa maana hiyo simu wamezipata kwa njia ambayo siyo halali,” ameeleza Mutafungwa.

Amewataja mafundi wanaoshikiliwa na jeshi hilo kuwa ni Musa Yusuph(29), mkazi wa Kitangiri, Patrick Herman((24) makazi wa Iseni, wamekatwa na simu pamoja na vifaa mbalimbali wanavyobadilisha kutoka kwenye simu za wizi  wanazo pokea kutoka kwa wezi mbalimbali wa simu za mkononi baada ya hapo  kuzibadilisha  wanaamua kuuza kwa wateja wao wanao wafahamu.

Watuhumiwa wengine ni Mecktrida Samweli(29),Mkazi wa Nyegezi na mfanyabiashara ambaye amekamatwa na simu 28, Liberty  Coasta(50) mkazi wa Nyamanoro ambaye amekamatwa na simu 16,Allen  Bwire(28) amekamatwa na simu 12,Ali Abdallah (27) fundi simu amekamatwa na simu 5,Chacha Maliba(40),mkazi wa Bugarika amekamatwa na simu 72, Jonas Benard(23) amekamatwa na simu 6.

Wengine ni Robert  Rongino (33),mkazi wa Mahina amekutwa na simu 39,Evodius Renatus (28),mkazi wa Kiloleli amekutwa na simu 16,Edson Kaponko(45), amekamatwa na simu 35 pamoja na  Magodi Mtundi(35) amekamatwa na simu 80.

 Mutafungwa ameeleza kuwa watuhumiwa wamehojiwa kwa kina na  watafikishwa mahakamani upelelezi utakapo kamilika huku akitoa onyo kwa watu wote wanaojihusisha na matukio ya wizi wa simu jijini Mwanza na operesheni inayoendelea haita waacha salama lazima watakamatwa na kuchukuliwa hatua.

Pia ametoa wito kwa watu wanaojihusisha na ununuzi wa vitu vya wizi waache tabia hiyo mara moja aidha kwa watu wote wanaotaka kuwa na simu,kununua au kumiliki  wakanunue kwenye maduka yanayo fahamika kuliko kununua katika uchochoroni na kununua vitu ambavyo vimeoatikana kwa njia isiyo halali kwani kwa kufanya hivyo wanazidi kuchochea wizi katika maeneo mbalimbali.

“Kuzuia uhalifu ni jukumu letu sote na kuzuia uhalifu ni pamoja na kuacha kupenda kununua vitu vya mteremko kama simu inathamani kubwa unataka mteremko unanunua kwa gharama ndogo kwa vyovyote simu hiyo itakuwa imepatikana kwa njia ambayo siyo halali,wananchi acheni kununua vitu vya mteremko vya wizi,”.