Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
BALOZI wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Tanzania katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii (UN Tourism), Mhe. Saidi Yakubu, amewasilisha hati zake za utambulisho kwa Katibu Mkuu wa Shirika hilo, Bi. Shaikha Al Nuwais, jijini Madrid, Hispania.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao wamejadili kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na UN Tourism, hususan kuwajengea uwezo watumishi na wadau wa sekta ya utalii, pamoja na kupata msaada wa kiufundi na kitaalamu katika kubuni na kuendeleza bidhaa na vivutio vipya vya utalii nchini.

Al Nuwais amepongeza ushiriki wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika filamu ya Tanzania: The Royal Tour, akitambua mchango wake katika kuitangaza Tanzania kimataifa. Ameeleza pia kufurahishwa na takwimu zinazoonesha ukuaji wa utalii nchini.
Tanzania, ambayo kwa sasa ni mjumbe wa Baraza la Utendaji la UN Tourism, inaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ili kupanua fursa za utalii, kuongeza ushindani wa sekta hiyo na kukuza mchango wake katika uchumi na ajira.

More Stories
Waziri Chande azindua bweni la Wasichana Chuo cha BTI
TTCL yafungua milango ya Kidijitali kwa Watanzania
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufungua kliniki ya Sheria Arusha