



Joyce Kasiki, Mbeya
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha ustahimilivu wa Taifa dhidi ya majanga kupitia utekelezaji wa sera, sheria, mikakati na miradi mbalimbali.
Amesema hatua hizo zinalenga kujenga ustahimilivu wa jamii dhidi ya maafa kwa ajili ya kuokoa maisha, mali, na rasilimali za taifa. Ameyasema hayo leo Jumatatu, Oktoba 13, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa City Park Garden, Mbeya, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Madhara ya Maafa.
Majaliwa ametaja hatua zilizochukuliwa ikiwa ni pamoja na kuandaa na kuhuisha nyaraka za kitaifa kuhusu maafa kama vile Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa (2025), Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa (2022–2027), na Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa (2022).
Aidha, amesema Serikali imeimarisha usahihi wa utabiri wa hali ya hewa kupitia TMA ambao umefikia asilimia 85, na hivyo kusaidia kupunguza madhara ya maafa kwa zaidi ya asilimia 30.
Serikali pia imetumia teknolojia za kisasa kuweka mifumo ya tahadhari ya mapema, ikiwemo kuanzishwa kwa Kituo cha Ufuatiliaji wa Majanga na Utoaji wa Taarifa kilichounganishwa na vituo vya kikanda barani Afrika.
Majaliwa ameongeza kuwa miradi mikubwa ya kimkakati yenye kuzingatia mabadiliko ya tabianchi inatekelezwa, kama vile ujenzi wa Bwawa la Kidunda (Tsh bilioni 329.47), Bwawa la Farkwa (Tsh bilioni 312.08), na Mradi wa Maji Ziwa Victoria–Simiyu (Tsh bilioni 440).
Katika sekta ya kilimo, amesema Serikali inaendeleza mbinu za ustahimilivu kwa kuboresha kilimo cha umwagiliaji, matumizi ya mbegu bora, mifumo ya tahadhari ya mapema, na kushirikiana na wakulima wadogo.
Pia Serikali imeendelea kulijengea uwezo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kuwekeza kwenye vifaa, teknolojia na mafunzo ya kisasa ili kuboresha huduma za uokoaji na uzimaji moto.
Ametoa wito kwa sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika uwekezaji unaozingatia ustahimilivu dhidi ya majanga, ikiwemo kuweka bima na kutekeleza miongozo ya Serikali.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, amesema lengo la maadhimisho ni kuhamasisha ushiriki wa wadau wote katika usimamizi wa maafa, huku Umoja wa Mataifa ukieleza kuwa taasisi mbalimbali zinaendelea kushirikiana kwa ukaribu katika maandalizi na kukabiliana na majanga.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama