January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

10 kuiwakilisha Tanzania mashindano ya dunia Slovenia

Na Ester Butabile, TUDARCo

NYOTA 10 waliofanikiwa kufanya vizuri katika mashindano ya UMITASHUMTA katika upande wa Riadha wanaendelea na kambi Mkoani Mtwara kwa ajili ya maandalizi ya awali ya mashindano ya Kimataifa ya Shirikisho la Michezo ya Wanafunzi Duniani (ISSF) yatakayofanyika Septemba 2021 nchini Slovenia.

Kambi hiyo ya awali itadumu kwa siku kadhaa kabla ya kuvunja ili kuwapa fursa wanafunsi hao kwenda katika shule zao kuendelea na masomo na mwanzoni mwa mwezi Agosti wataingia tena kambini kwa ajili ya mashindano hayo.

Akizungumza naMtandao huu, Mratibu wa UMITASHUMTA na UMISSETA Taifa, Leonard Thadeo amesema kuwa, katika uteuzi wa wachezaji hao 10 walizingatia kanuni na sheria zote za mchezo kwani mbali na nidhamu pia waliangalia nidhamu ambayo ni moja ya sifa itakayowawezesha kupeperusha vema bendera ya nchi ya Taifa na kuitangaza zaidi nchi kama wanavyofanya wanariadha wakumbwa Alphonce Simbu, Failuna Matanga na Gabriel Geay watakaoiwakilisha nchi kwenye michuano ya Olimpiki, 2021.

Amesema, baada ya kambi hiyo ya awali wanafunzi hao watarudi shule kuendelea na mazoezi na Agosti wataingia rasmi kambini ili kufanya maandalizi kwa ajili ya michuano hiyo itakayoanza kutimua vumbi Septemba.

“Hii ndiyo dhana ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa ya kutaka ufundishaji michezo kuanza kwenye shule za Awali, Msingi, Sekondari na Vyuo ili kupata washiriki wengi walionolewa vizuri kwenye mashindano ya kimataifa kama yanavyofanya mataifa makubwa,”.

“Lakini pia wakati anafungua UMITASHUMTA alisema kuwa, kupitia michezo na sanaa, wanafunzi watafunguliwa vipaji vyao ambavyo vikiendelezwa vema vitawapatia manufaa mazuri ya kitaaluma na ajira na tunaamini hii itakuwa mwanzo wa safari ya vijana hawa kimataifa,” amesema kiongozi huyo.

Itakumbukwa kuwa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasim alisisitiza kuwa, Serikali imejipanga kuanzisha na kuboresha  vyuo vya michezo nchini ili  kupika na kunoa vipaji  vya wanamichezo ambavyo vitaweza pia kuuzwa duniani.

“Mikakati ya Serikali kwenye Sekta ya Michezo kwa sasa ni kuhahakisha taaluma ya michezo inaboreshwa na inatolewa kwa kiwango cha kimataifa ili wanamichezo wetu wawe kwenye viwango vya kimataifa, tukumbuke kuwa michezo ni sayansi,” amesema Dkt. Abbasi.