Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.
SIKU nne zilizotengwa na serikali kwa wadau mbalimbali wakiwemo vongozi wa dini, pamoja na vyama vya siasa nchini Tanzania kutoa maoni yao kuhusu Miswada minne ya Bunge iliyosomwa kwa mara ya kwanza wakati wa Mkutano wake wa 13, zimekamilika leo Januari 10,2024.
Miswada hiyo ni pamoja na ule wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2023, Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa Mwaka 2023 pamoja na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.5) wa Mwaka 2023 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No.5) Bill, 2023].
Muswada mwingine ni ule wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa Mwaka 2023 [The Political Affairs Laws (Amendment) Bill, 2023].
Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na sheria Joseph Mhagama aliwaambia waandishi wa habari kuwa wadau wamejadili maudhui na kero zinazohusu maudhui hayo huku akikiri uwepo wa maoni yaliyo nje na mjadala tarajiwa.
Kulingana na Mhagama, zoezi hilo limeshirikisha Watanzania wote wenye maslahi kwenye masuala ya uchaguzi na siasa za ndani ya nchi.
Pia, aliwahakikishia Watanzania kuhusu kusikilizwa na kufanyiwa kazi kwa maoni yote yaliyotolewa na makundi hayo.
“Maoni ambayo yatachukuliwa ni yale ambayo hayavunji Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pili yanaboresha miswada iliyopo,”amesema kiongozi huyo wa kamati.
Baadhi ya wadau walioshiriki zoezi hilo muhimu kwa mustakabali wa nchi, wameangazia maeneo yanayopaswa kupewa kipaumbele kwa maslahi ya taifa.
Naye Katibu Mkuu wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema John Mnyika amependekeza kuondolewa kwa baadhi ya vipengele hasa, vinavyohusu uchaguzi pamoja na kile kinachotoa nafasi kwa wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia uchaguzi kwa kile alichokisema ni ‘kutokuwa na tija kwa vyama vya upinzani.’
Mnyika, ambaye ni mbunge wa zamani wa majimbo ya Kibamba na Ubungo, amesema upinzani haukubaliani na muundo wa Tume uliopendekezwa kwenye sheria ambayo inaundwa na Rais, ambaye pia ni sehemu ya wagombea. Badala yake, Chama hicho kimependekeza sheria iweke wazi kuwa Tume iwe na wajumbe wenye uwakilishi bungeni.
Hatua hii inakuja wakati Tanzania inatarajia kuingia katika uchaguzi mdogo wa Serikali za mitaa baadaye mwaka huu na kutoa fursa ya kufanyika kwa uchaguzi Mkuu wa kitaifa utakaohusisha mihimili ya bunge na Utawala, ifikapo Oktoba 2025.
Ambapo Zoezi hilo limekamilika baada ya kuhusisha vyama 18 vya siasa vilivyosajiliwa, taasisi za dini, wananchi na asasi za kiraia zaidi ya 400.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa