December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe,

Zitto aweka wazi Watanzania wakavyonufaika na bima ya afya

Na Mwandishi Wetu, TimesMjira Oline

CHAMA cha ACT-Wazalendo,kimeelezea hatua zitakazochukuliwa na chama hicho na washirika wake pindi kikichukua dola katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana amesema katika Ilani ya chama hicho, wameeleza kwa kina ni namna gani kitawezesha kila Mtanzania kuwa na bima ya afya ifikapo mwaka 2025

Zitto amesema Serikali ya chama hicho na washirika wake wataunganisha mfumo wa hifadhi ya jamii na Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa (NHIF) ambapo kila mwanachama wa Skimu ya Hifadhi ya Jamii atapata Fao la Bima ya Afya litakalosimamiwa na NHIF.

Amesema hapatakuwa na michango tofauti ya Bima ya Afya na Hifadhi ya Jamii. “Kila Mtanzania ambaye ni mkulima, mfugaji, mvuvi, mfanyabiashara ndogo ndogo au mtu yeyote asiye kwenye sekta rasmi atachangiwa na Serikali nusu ya mchango wa kima cha chini cha kuchangia kwa mwezi kwenye Hifadhi ya Jamii,” alisema Zitto na kuongeza;

Kwa mujibu wa Zitto, mtu atakayechangia kwa miaka 10 mfululizo kwenye Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii atakuwa na sifa ya kulipwa Pensheni atakapokuwa na umri wa kustaafu uliowekwa na Serikali.

“Akifariki dunia kabla ya kutimiza miaka 10 michango yake na riba italipwa kwa warithi wake. Akitaka kujitoa kabla ya miaka 10, atalipwa kiasi alichochangia na riba. Akijitoa baada ya miaka 10 atalipwa pesa yote iliyo kwenye Akaunti yake ya Skimu ya Hifadhi ya Jamii ikiwemo mchango wa Serikali,”amesema Zitto.

Alisema Bima ya Afya, Fao za Uzazi kwa wanachama wanawake, Fao la Bei kwa Wakulima, Bima ya Mazao, Samaki/Dagaa na Mifugo na Mikopo kwa Vyama vya Ushirika na jumuiya za wananchi itakuwa ni sehemu ya mafao ya muda mfupi kutoka Skimu ya Hifadhi ya Jamii ya Taifa.

Kwa mujibu wa makadirio ya idadi ya watu wazima nchinina ukuaji wa idadi ya watu, na kwa kuzingatia kiwango cha chini cha kuchangia cha sh. 30,000 kwa mwezi kwa kila Mtanzania; gharama za mchango wa Serikali (MATCHING FUNDS) kwa Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa watu walio nje ya Sekta Rasmi ili kila Mtanzania kuwa na bima ya afya inakadiriwa kufikia sh. bilioni 648 kila mwaka.

“Fedha hizi zitatoka kwenye Bajeti ya Serikali ya Kila Mwaka kwa Mujibu wa Sheria Maalumu itakayotungwa na Bunge,”amesema.

Kuhusu faida ya mfumbo huo, Zitto amesema utarahisisha malipo ya hifadhi ya jamii na bima ya afya kwa mwananchi kuchangia mara moja tu kwa chombo kimoja tu.

“Ukiwa na kadi ya hifadhi ya jamii moja kwa moja unakuwa na bima ya afya, bima ya mazao kwa wakulima na mima ya majanga kwa wakulima, wavuvi na wafugaji.

Wafanyakazi watachanga mara moja tu badala ya sasa ambapo wanalipa Hifadhi ya Jamii na pia wanalipa Bima ya Afya,” amesema na kwamba mfumo huo utatoa kivutio kwa wananchi wengi kujiwekea Akiba kwani kila sh. 1 wanayoweka Serikali pia inawawekea sh. 1 nyengine.

Amesema uwiano wa uwekaji akiba nchini kwa Pato la Taifa utaongezeka na hivyo kuwezesha uwekezaji mkubwa wa kuongeza shughuli za uchumi kuongezeka.

Zitto amesema uwekezaji wa ndani utakua kwa kasi na hivyo nchi kuweza kutekeleza miradi mikubwa ya uzalishaji mali inayochukua muda mrefu kuanza kuzalisha faida kama vile kilimo cha umwagiliaji, viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, uvuvi na mifugo.

“Kila Mtanzania atakuwa na Bima ya Afya kwani mtu mmoja wanachama wa hifadhi ya jamii anachangia watu 5 kwenye Bima ya Afya. Skimu ya Hifadhi ya Jamii ya Taifa ikifikisha watu milioni 10, itakuwa ni sawa na Watanzania milioni 60 kuwa na Bima ya Afya,” amesema.