Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Cairo
ZIARA iliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Misri Novemba mwaka 2021, imezaa matunda baada ya kampuni ya Elsewedy kukubali kuja kujenga kongani ya viwanda Mlandizi Mkoa wa Pwani.
Wakati wa ziara yake nchini humo, Rais Samia na ujumbe wake alitembelea Kongani ya Viwanda ya Kampuni ya ElSewedy ambapo aliishawishi Kampuni hiyo kuanzisha Kongani kama hiyo nchini Tanzania.
Katika kutekeleza agizo la Rais Samia baada ya kuwashawishi ElSewedy kujenga Kongani kama hiyo nchini, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimeendelea kufanya mawasiliano ya karibu na wawekezaji hao.
Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri, hivi sasa yuko ziarani nchini Misri kwa kazi hiyo ambapo amekutana na kufanya kikao kazi na Kampuni ya ElSewedy na tayari wamekubali kuja kujenga mji wa viwanda Tanzania (Egyptian Industrial City) eneo la Mlandizi, mkoani Pwani.
Teri amesema wawekezaji hao wa Misri wataleta Kongani zao nchini Tanzania katika sekta mbalimbali huku sekta kubwa ambayo itapewa kipaumbele ni sekta ya viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu (Pharmaceutical industries).
Katika ziara hiyo ya TIC nchini Misri, Mkurugenzi Mtendaji, Teri alikutana na uongozi wa Kampuni ya Utopia Pharmaceuticals ambao wameahidi kuwekeza kiasi cha Dola za Marekani Milioni 100 kwa miaka 10 ijayo katika ujenzi wa viwanda hivyo vya dawa za binadamu nchini Tanzania.
“Hawa Utopia Pharmaceuticals watawekeza kiasi hicho cha fedha, Dola za Marekani Milioni 100 kwa miaka 10, lakini wataanza na Dola za Marekani Milioni 10 miaka miwili ya mwanzo na wataleta viwanda vya Dawa za Binadamu aina 10 zinazohitajika sana nchini,” alisema Teri.
Aidha, Teri amesema wawekezaji hao tayari wamesajili biashara nchini Tanzania na wako katika hatua za mwisho kukamilisha taratibu kwa ajili ya umiliki wa ardhi nchini ili waweze kujenga viwanda hivyo na hatua ya kwanza katika uwekezaji huo wataanza kujenga hala kubwa la dawa (Medical Warehouse).
Teri ameleza kuwa, ujenzi wa Kongani hizo nchini Tanzania utaleta manufaa mengi ikiwa ni pamoja na Kampuni za Misri kushirikiana na Kampuni za Tanzania katika uanzishwaji wa Viwanda vya aina mbalimbali.
“Watanzania wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo kushirikiana na wawekezaji wenzao wa Misri, pia Watanzania watapa ajira kupitia viwanda hivyo na biashara hizo za pamoja, zitapunguza uagizwaji wa dawa nje ya nchi,” alisema Teri.
Tanzania inatumiua kiasi cha Dola za Marekani bilioni moja kuagiza dawa nje ya nchi kila mwaka hivyo ujenzi wa Kongani ya Viwanda itasaidia sana kuongeza fedha za kigeni na kupunguza utegemezi wa kuagiza dawa kutoka nje ya nchi.
Kadhalika, ujenzi wa viwanda vya dawa utaiwezesha Tanzania kuuza dawa hizo kwenye nchi za Jumuiya za Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
More Stories
Kyobya: Watakaohusika kudhoofisha jitihada za Serikali,Pori la Akiba Kilombero kushughulikiwa
Wenje:Tuwanadi wagombea bila kuchafuana
Mtoto darasa la tatu adaiwa kujinyonga kwa kukosa nguo ya sikukuu