November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ziara ya Rais Samia kuimarika kwa utalii tiba

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

WAKALA wa Elimu Nje ya Nchi Global Education Link (GEL) imetaja fursa kem kem ambazo Tanzania itanufaika nazo kupitia ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan anayotarajia kuifanya nchini India ikiwemo kuimarika kwa utalii tiba nchini.

GEL imesema India ni nchi inayoongoza duniani kwa utalii tiba hivyo ziara ya Rais Samia itazidi kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na nchi hiyo kwenye sekta mbalimbali hususan afya.

Aliyasema hayo jana wakati akizungumza kwenye kilele cha wiki ya huduma kwa wateja iliyofanyika kwenye ofisi za wakala, jijini Dar es Salaam.

Mollel alisema ziara ya Rais Samia inayotarajiwa kufanyika nchini India kuanzia kesho Jumapili itakuwa na manufaa makubwa kwani Tanzania kwani nchi hiyo inawatalamu bobezi wa kila nyanja na ni nchi inayoongoza duniani kwa utalii tiba.

Alisema Tanzania imeshaazimia kuwa kitovu cha utalii tiba kwa nchi za kusini mwa jangwa la sahara hivyo ziara hiyo itaendelea kuimarisha uhusiano ambao utasaidia nchi kupata watalii wengi wa tiba.

“Kwenye upande wa elimu tutafunguliwa fursa nyingi sana za kwenda kusoma nje India, ufadhili wa wanafunzi utaongezeka, madaktari bingwa na bobezi ambao wanahitaji kubadilishana uzoefu na wenzao wa India fursa zitaongezeka,” alisema Mollel

“Pia tutafanya kitu kinaitwa reverse medical tourism kwa maana kwamba unaweza kuwa na miundombinu ya kutosha lakini ukakosa mabingwa sasa kupitia ushirikiano wa India na Tanzania mabingwa kutoka nchini humo watakuja kuungana na wa kwetu hapa na watatibu maradhi ambayo walikuwa wakienda kutibiwa nje ya nchi,” alisema Mollel

Aidha, alisema kwa uwekezaji ambao umefanywa kwenye sekta ya afya na serikali ya awamu ya sita na uhusiano mzuri wa Tanzania na India, nchi za Afrika Mashariki na kusini mwa Afrika zitaitegemea Tanzania kwa tiba za kibingwa.

Mollel alisema ziara hiyo pia itafungua milango kwa wanafunzi wa Tanzania waliosoma Shahada ya kwanza ambao wanataka kwenda India kusomea ubobezi kwenye fani ya afya na fani zingine.

“India inafahamika dunia nzima kwa ubobezi kwenye sekta ya afya kwa hiyo uwepo wa Rais wetu nchini India utasaidia kuimarisha ushirikiano wa vyuo vikuu vya nchi hiyo na vya hapa nchini ambavyo tumekuwa tukifanya navyo kazi kwa muda mrefu,” alisema

Alisema vyuo vingi vya India vina program za wanafunzi kusomea nchini humo na kumalizia kwenye vyuo vya mataifa mengine hivyo alisema hiyo ni fursa kwa vyuo vya hapa nchini kubadilishana wanafunzi na vyuo vya India.

Wakati huo huo, Molle alisema (GEL), imefungua dirisha kwa wanafunzi wanaotaka kwenda kusoma nje ya nchi muda wowote kwa muda wa mwaka mzima kuanzia sasa.

“Kwa wanafunzi waliokosa masomo vyuo vya ndani na nje ya nchi kuanzia sasa tumefungua dirisha la masomo na watakwenda muda wowote hatutafunga kwa yeyote anayetaka kwenda nje ya nchi aje tutamfanyia mchakato atakwenda ndani ya muda mfupi,” alisema Mollel

Alisema mwanafunzi yeyote ambaye amekosa udahili kwenye vyuo vya ndani asifikiri kwamba amechelewa kwani vyuo vya nje vitaendelea kupokea wanafunzi muda wowote watakaohitaji kwenda nje ya nchi.

Kadhalika, Mollel alisema GEL imejipanga kuongeza fursa za masomo kwa watanzania wanaotaka kwenda nje ya nchi kusomea ubobezi kwenye Shahada za Uzamivu (PhD) na Shahada za Uzamili.

Alisema kwa sasa asilimia 90 ya wanafunzi wanaokwenda nje ya nchi kusoma kupitia GEL ni wa Shahada ya Awali na ngazi za vyeti na Astashahada hivyo kuanzia sasa GEL itajitahidi kuongeza fursa za wanaotaka kusomea ngazi za juu za elimu.

Mbali na hivyo, alisema kutokana na mazingira mazuri ya elimu yaliyowekwa nchini, Tanzania itaanza kupata wimbi kubwa la wanafunzi kutoka nje ya nchi wanaokuja kusoma vyuo vya hapa nchini.