December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ziara ya Rais Samia Korea kuleta Trilioni 6.5

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mh. January Makamba amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuanza ziara ya siku saba nchini Korea Kusini kuanzia Mei 31 kwa mwaliko rasmi wa kiongozi mkuu wa taifa hilo.

Waziri Makamba ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa habari kwenye ofisi za Wizara hiyo zilizopo Jijini Dar, ambapo amesema ziara ya Rais Dkt. Samia itakuwa na sehemu kuu mbili, moja ni ziara rasmi kati ya Serikali ya Tanzania na Korea, lakini la pili ni Rais Samia kuhudhuria mkutano mkuu wa nchi za Afrika na Korea utakaofanyika Juni 3 na Juni 4.

Waziri Makamba amesema katika ziara hiyo ya Rais Samia, Serikali ya Tanzania itaingia mikataba saba ukiwamo wa msaada na mkopo nafuu wa Dola za Marekani 2.5 bilioni kutoka katika Serikali ya Korea Kusini.

‘Makubaliano hayo ni mapya ya ushirikiano wa maendeleo ya kati ya Serikali ya Tanzania na Korea na mkataba mkubwa kati ya mikataba saba Serikali itakayoingia na fedha hizi zitakwenda uboreshaji wa sekta ya elimu, afya na miundombinu’ – Waziri Makamba.

Waziri Makamba ameitaja mikataba mingine itakayosainiwa ni pamoja na ushirikiano katika maendeleo ya uchumi wa buluu, kutambua vyeti ya mabaharia, tamko la pamoja la uanzishwaji wa majadiliano na mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi.

Mingine ni hati ya makubaliano kati ya Taasisi ya Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Taasisi ya Sayansi na Miamba na Madini ya Korea, ushirikiano utakaojikita katika utafiti, uchoraji ramani, rasilimali na shughuli za maabara.

Mbali na hilo, Waziri Makamba amesema kutakuwa na hati ya makubaliano kati ya Wizara ya Madini ya Tanzania na Wizara ya Viwanda na Biashara ya Korea kuhusu ushirikiano wa kuchambua na kufanya utafiti wa madini mkakati.

Halikadhalika kutasainiwa mkataba wa makubaliano kati ya Shirika la Taifa la Madini (Stamico) na Shirika la Ukarabati wa Migodina Rasilimali za Madini la Korea.

Waziri Makamba amesema ziara hiyo, pia itaanzisha ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Korea cha Usafiri wa Anga na Tanzania ili kuboresha soko la usafiri wa anga na uendeshwaji wa biashara ya sekta hiyo.Pia uendeshaji na uratibu wa viwanja vya ndege, utalaamu,utafiti na huduma.

Mbali na hilo, Waziri Makamba amesema kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye menejimenti ya usafiri wa anga nchi ikiwemo miundombinu ya ukabarati na ujenzi wa viwanja na udhibiti na ufufuaji wa usafiri wa anga.

Chuo Kikuu cha Masuala ya Anga cha Korea kitamtunuku Rais Samia shahada ya heshima ya udaktari katika menejimenti ya usafiri wa anga.

Katika hatua nyingine,Waziri Makamba amesema Rais Samia atashiriki mkutano wa wakuu wa nchi kati ya Korea na Afrika utakaoanza Juni 3 hadi 4 na mkuu huyo wa nchi atapata nafasi ya kuhutubia na kuzungumza katika jopo moja kati ya manne yatakayokuwapo.