November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ziara ya Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo, Mkoa wa Dar es salaam kuzungumza na Halmashauri Kuu za Wilaya ya Ubungo na Kinondoni

Tupo kwenye uchaguzi Mkuu wa Ndani, sasa ni ngazi ya mashina taratibu na katiba ya chama chetu inatoa fursa na haki kwa kila mwanachama kuchagua na kuchaguliwa, kitu ambacho kinanisikitisha kuna baadhi ya maeneo wanachama wananyimwa fursa hiyo, tena wananyimwa kwa makusudi, kwa hapa Dar es salaam kuna maeneo kama Tandika, Manzese, kimara, baadhi ya makatibu wa matawi kwa sababu wana maslahi yao binafsi wanawanyima baadhi ya wanachama kuchukua fomu kwa kuwaambia fomu zimeisha na hawawapatii ili wawapitishe watu ambao wanafikiri watasimamia maslahi yao, hili ninalipiga marufuku.

“Naawagiza Makatibu wa wilaya, Ubungo na wilaya zote nchini, maeneo yote ambayo tumebaini yana changamoto ya watu kunyimwa kuchukua fomu za kugombea ndani ya chama, tunarudisha zoezi la kutoa fomu, tunataka wale wote wenye dhamira ya kuchukua fomu wachukue bila kuwekewa vizuizi, hiki sio chama cha mtu, hiki sio chama cha maslahi binafsi, hiki chama ni cha wanachama, na ni lazima tutende haki kwa kuwa katiba yetu ya CCM inatutaka tufanye hivo.”

“Dhamana tulizonazo hazijatupa haki ya kufanya maamuzi kwa ubinafsi, maeneo ambayo tumegundua yana hiyo changamoto wawaruhusu watu wachukue fomu, kura zisismame kwenye hayo maeneo watu waruhusiwe kuchukua fomu ili watendewe haki ya kuchaguliwa”

“Kuna maneno, hapa Ubungo, Babati, Mbeya, Sehemu ya Tabora, watu wamechukua kadi wanakwenda kuwapa watu ambao wanataka watumike kuwapigia kura, naagiza kwa makatibu wa wilaya Nchini, vitabu vilivyokuwa vimehakikiwa ndio vitumike kwenye kupiga kura na sio vinginevyo, tutafuatilia na tukibaini kuna maeneo ambapo vitabu vilivyokuwa vimehakikiwa vimeongezwa majina wakurugenzi (Makatibu) wa uchaguzi watawajibika, hili sihitaji kusisitiza tutakutana baadae na hili ni kwa ngazi zote.”

“Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi, vijana wa hamasa nchini hamkuzaliwa kuwa vijana wa hamasa tu, kazi mnazofanya ni nzuri sana na huu ni wito wangu kwa vijana wote nchini, acheni kubakia kuwa wapambe tu wa wagombea, na mkiona kuna mazingira ambayo yanataka kuwafungia milango tuambiane haraka sisi tunafunguo”

“Ninawaagiza wenyeviti na makatibu wa vijana nchi nzima, kwenda kukaa na vijana kuwahamasisha kugombea na hilo ni jukumu na wajibu usio na hiyari, lazima tuwapatie fursa vijana kuingia na kutumia haki zao za msingi za kuchaguliwa kwa sababu na wao ni wanachama na wanahaki ya kuingia na kutoa mchango wao kwa nchi yao.”