Na Mwandishi wetu, Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeiunga mkono Kampuni ya Airpay Tanzania katika adhma yake ya kutoa huduma za uhakika za malipo ya fedha kwa njia ya kidigitali kwa kuahidi kushirikiana nayo katika kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa na linaanza kwa muda uliopangwa.
Akizungumza leo visiwani Zanzibar, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji ,Mudrick Ramadhani Soraga wakati Benki Kuu ya Tanzania Ofisi ya Zanzibar ikiikabidhi leseni kwa Kampuni ya Airpay Tanzania tukio lililoenda sambamba na ufunguaji rasmi wa ofisi ya kampuni hiyo iliyopo Mlandege, Zanzibar.
Amesema serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa kampuni hiyo kwa sababu imekuja na teknolojia ya hali ya juu ambayo itakuja kufanya mageuzi makubwa ya Tehema ndani ya nchi.
Soraga amesema teknolojia hiyo siyo tu itawanufaisha wajasirimali wadogo bali itanufaisha hata benki na watoaji huduma wengine mbalimbali wa malipo nchini.
“Hii ni kampuni ambayo ina uzoefu na biashara kwa zaidi ya miaka 12, kikubwa kama Serikali tutawapa ushirikiano wa hali ya juu ili zile huduma ziweze kupatikana kwa wananchi, tumekubaliana kwamba ni muhimu wakabaki katika misingi yao hasa kuwaangalia wajasiriamali wadogo, wa kati na hatimaye wale wakubwa,” amesema
Aidha amesema Airay Tanzania ni kampuni ya kwanza kuweka makao yake makuu visiwani Zanzibar ikiwa ni moja ya mkakati wa Serikali katika kuvutia wawekezaji katika masuala ya Tehama na masuala mazima ya mifumo.
“Nawapongeza Airpay kwa kuamua kufanya maamuzi mazito ya kuwekeza Zanzibar na kuifungua kama kitovu cha uwekezaji wa mifumo ya Tehama na sehemu ambayo itajulikana duniani kwamba inakaribisha kampuni mbalimbali ya Tehama,” amesema
Naye Kamishna wa Idara ya Mashirikiano baina ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), Dk. Bili Mrima Kiwia amesema wanaiunga mkono kampuni hiyo kwa sababu itaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za malipo kwa njia ya mtandao kwa wananchi.
“Kampuni hii inajihusisha na mifumo mbalimbali ya malipo na wapo kuangalia ni kwa namna gani wataweza kuunganisha mifumo iliyopo kwa lengo la kurahisisha ufanyaji wa biashara ili kuweza kuwasaidia wajasiriamali wadogo wadogo waliopo Zanzibar kuweza kufanya biashara pamoja na kukopesheka,” amesema
Aidha Meneja Uchumi Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ofisi ya Zanzibar, Moto Lugobi amesema wametoa leseni kwa kampuni hiyo baada ya kujiridhisha kuwa itatoa huduma hiyo kwa misngi waliyokubaliana.
Kwa upande wake Mwanzilishi wa Kampuni ya Airpay, Kunal Jhunjhunwala amesema mtazamo wa kampuni hiyo ni kutoa huduma bora na za uhakika kwa Zanzibar na Tanzania bara kwa ujumla.
“Zanzibar ni mdau sahihi wa kushirikiana naye hasa katika kulasimisha mifumo ya kidigitali, tumevutiwa na serikali hii kwa sababu haichelewi kufanya maamuzi, tumejipanga kuhakikisha tunatoa huduma bora kwa njia ya kidigitali, hivyo watanzania walipo Visiwani Zanzibar na Bara watupokee kwani watapata huduma nzuri kwa wakati,” amesema Jhunjhunwala
More Stories
Mwanasheria Mkuu apiga kura uchaguzi wa serikali za mitaa
CHADEMA yasikitishwa mawakala wao kuzuiliwa
Rais Samia amlilia Dkt. Ndugulile