Na Mwandishi wetu,TimesMajira,Online,Dar
WAKULIMA wa mpunga Wilaya ya Mbarali wamesema jitihada ya Serikali ya kupeleka zana za kisasa za kilimo wilayani humo inachochea ari ya wanavijiji kulima mpunga kwa wingi na huenda watu wakafikiria kulima hata mahindi.
Wakizungumza na waandishi wa habari za kilimo jijini hapa hapa baadhi ya wakulima waliohudhuria Maonyesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Saba Saba), wamesifu jitihada ya sasa ya serikali ya kuhimiza kilimo na jitihada ya makusudi ya kupeleka zana bora vijijini ili kuboresha kilimo na kupunguza adha katika ulimaji na uvunaji
Amos Mwangulube aliotoa mfano wa kupelekwa kwa kombaini havesta15 katika Chama cha Ushirika cha Msingi cha Nguvu Kazi ya Wanavala, wilayani Mbarali na kusema hatua hiyo itachochea sana ulimaji wa mpunga kwa sababu uvunaji utakuwa mwepesi na mpunga hautopotea shambani.
Chama hicho kimepata zana hizo kutokana na mkopo wa masharti nafuu wa sh. milioni 950 uliotolewa na Benki ya Kilimo Tanzania (TADB).
“Sisi tumezoea kulima kwa plau na jembe na kuvuna kwa kisu. Wenye uwezo wanalima kwa matrekta. Lakini kombaini havesta walizopata Wanavala zitasaidia wakulima wengi maana wanaweza kuzikodisha au kuwaazima wakulima wengine wakati wa mavuno,” amesisitiza.
Amedai kuwa upelekaji wa mashine hizo Mbarali umechochea ari ya kulima mpunga kwa kuwa zana hizo zitarahisisha sana uvunaji wa mazao kama mpunga na mahindi.
“Kazi ya kuvuna kwa taabu na kwa muda mrefu sasa inakariba kwisha katika eneo letu na hatutapoteza tena mpunga wetu shambani,”ameeleza na kuongeza kuwa zana hizo pengine wataazimwa kwa wakulima wa mpunga wa wilaya nyingine kama Kyela. “Kyela nao ni walimaji wakubwa wa mpunga,” amesisitiza.
“Nina ndugu zangu hapa Dar es Salaam kwa hiyo nimehudhuria maonesho ya SabaSaba kwa nia ya kupata wateja wa mchele wetu hapa Dar es Salaam. Watu wa Dar es Salaam wanapenda sana mchele wa kwetu.
Tuna mpango wa kutafuta wauuzaji wa jumla na rejareja wa Dodoma maana watu wanaongezeka sana huko Dodoma,” ameeleza.
Amesema ana shamba la hekri sita katika mbonde la familia na humo ndimo amekuwa akilima mpunga kwa zaidi ya miaka 30. “Kulima mpunga ni kazi yetu na tuna ujuzi wa kulima zao hilo,” amesema.
Wukulima wa Mbarali wana uzoefu wa kulima kwa zana bora, badala ya jembe. Kwa mujibu wa takwimu za Serikali, wilaya ya Mbarali ndiyo ya juu kabisa (asilimia 3.1) katika kulimia power tiller, katika Mkoa wa Mbeya ikifuatiwa na Wilaya ya Mbeya Vijijini asilimia 0.9.
Kadhalika wakulima wa Mbarali ni wa pili katika kutumia plau asilimia 17.3% wakitanguliwa na wakulima wa Wilaya ya Momba asilimia 32.1.
Uzuri wa kombaini havesta ni kwamba vifaa vya uvunaji vinaweza kufunguliwa na kuwekwa kando, na trekta likatumika kulima na kufanya kazi nyingine.
Mwenyekiti wa Chama cha Umoja wa Wakulima Mpunga Mbarali, Wilbart Mbwiga, ameeleza kwa simu jana kwamba kwa kutumia kombaini havesta wanachama wote watahudumiwa kwa usawa wakati wa mavuno. “Jambo kubwa ni kwamba zana hizi zitumiwe kwa uangalifu sana ili zilete ufanisi na zidumu,” amesema.
Anangisye Mwangomale , mkulima mashuhuri wa mpunga amesema huvuna magunia saba katika hekta moja na kutabili kwamba uzalishaji wa mpunga utaongezeka wilayani humo na wilaya nyingine kutokana na uongezekaji wa zana za kisasa vijijini.
“Ari ya kulima mpunga inaongezeka. Si ajabu wakulima wengine wakaanza kulima mahindi,” ametabiri.
Wakati akihutubia Bunge, Rais Samia Hassan aliahidi kwamba Serikali itaendelea kuiimarisha TADB ili ishiriki kikamilifu katika kuongeza tija katika sekta ya kilimo.
Katika kuendeleza sekta ndogo ya mpunga tu, hadi kufikia mwezi jana TADB ilikwishatoa 5,601,149,821.75 kuendeleza mnyororo wa thamani katika zao hilo, zaidi za milioni 900 kwa kombaini havesta, 678,542,579.78 kwa kununulia matrekta, 799,991,071 kwa ajili ya maghala, na 1,349,138,016.75 kwa ajili ya mashine mbali mbali.
More Stories
Kilo 673.2,dawa za kulevya zakamatwa Bahari ya Hindi
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule
Wananchi Kisondela waishukuru serikali ujenzi shule ya ufundi ya Amali